Simulizi : Singidani Sehemu Ya Kumi naTano (15) Mwishoo

Simulizi ya singidani
Laura akanyanyuka na kwenda ndani, baadaye aliporejea alikuwa na karatasi yenye namba ya simu, akampa mumewe. Chris palepale akampigia Jully.

“Kaka ulisema nikutafute baada ya fungate lakini naona kama nachelewa sana kujua, ndiyo maana nimekutafuta mapema,” akasema Chris mara baada ya Jully kupokea simu.

“Usijali kaka, uko wapi?”

“Zanzibar, tunaweza kuzungumza sasa?”

“Siyo ya kwenye simu kaka, halafu napenda nikizungumza uwe na Laura.”

“Njoo Zanzibar basi, kila kitu nitagharamia mimi.”

“Kweli?”

“Ndiyo, tena ikiwezekana leo. Sema nifanye mpango wa ndege ya jioni mara moja.”

“Nakubaliana na wewe.”

Ndivyo ilivyokuwa, mipango ikafanyika vyema, jioni yake Jully aliingia Zanzibar. Aliungana nao kwenye hoteli ileile waliyofikia. Jioni wakiwa wanapata chakula, Jully akaanzisha mazungumzo...

“Kwanza hongereni kwa kufanikisha kufunga ndoa. Nataka kuwahakikishia kuwa, kila mmoja ni muhimu na maalum kwa mwenzake. Muishi kwa upendo, amani na kusikilizana.

“Pia nimefurahi kwamba, mimi ni mtu pekee mliyeniamini na kunipa heshima ya kuwatembelea hadi kwenye fungate yenu, ahsanteni sana ndugu zangu,” akaanza kusema Jully.

“Usijali kaka, tupo pamoja. Wewe ni mtu muhimu, maana bila wewe ilikuwa vigumu sana kumpata Laura.”

“Ni kweli. Ila kuna jambo ambalo lazima niliseme kwa ukweli wa moyo wangu, maana nisipofanya hivyo nitabaki na mateso makubwa sana moyoni. Hiyo ndiyo sababu iliyonifanya nifunge safari kutoka Moshi hadi Dar kufuatilia kuhusu harusi yenu na hatimaye nikahudhuria.

“Kuna jambo nimewafanyia, siyo zuri. Siyo la kiungwana hata kidogo, nataka kuwa mkweli kwenu, lakini nawaomba kabla sijaanza kusema, mkubali kunisamehe kwa nilichowafanyia kwanza,” akasema Jully, sasa akianza kutokwa machozi.

Wote wakamshangaa.

Jully akamgeukia Laura, akamwambia: “Laura tafadhali naomba unisamehe!”

Laura hakumjibu, akamgeukia mumewe na kumwangalia kwa makini, akamwonesha ishara kuwa, akubali kumsamehe ili wamsikilize mpaka mwisho.

Laura akatingisha kichwa.

“Ahsante. Je, Chris nawe utanisamehe?” Akauliza Jully.



“ENDELEA tu Jully, tupo hapa kwa ajili yako.”

Moyoni Chris alikuwa na mzigo wa mawazo lakini ilikuwa lazima ajue ni kitu gani alichotaka kusema Jully.

“Nashukuru sana. Sasa nipo radhi kuzungumza... mnakumbuka kuhusu ishu ya polisi Singida?” akauliza Jully.

Wote wakaonekana kuvuta kumbukumbu vizuri, hakuna aliyekumbuka haraka kuhusu jambo hilo.

“Sikia Jully, maadam umekubali kusema na umeshasema tukusamehe, sisi tupo tayari, huna sababu ya kutuchengesha tena. Sema ni nini?” akauliza Chris akiwa hajulikani kuwa alipandisha midadi tu au alikuwa amekasirika.

“Ni kweli. Kumbuka kuwa, ulifuatwa gesti uliyofikia Singida ukaambiwa kuwa unatembea na mke wa polisi, tena mkuu wa kituo, umeshakumbuka?” akauliza Jully.

“Ni kweli, nimekumbuka.”

“Mimi ndiyo nilihusika na mchezo wote ule,” akasema Jully kwa kujiamini.

Muda huohuo Jully akapiga magoti chini huku akilia...

“Nilifanya vile kwa tamaa tu. Nilitaka kutengeneza mchezo ili nipate fedha, lakini ikashindikana. Ni jambo linaloniumiza sana moyo wangu.

Ningeweza kukaa na hili jambo moyoni, lakini linaniumiza na kunitesa. Pamoja na kwamba tamaa yangu ilikuwa kwenye fedha tu, kumbe ningeharibu jambo zuri la ndoa ambalo mmeshalitimiza.

“Naombeni sana mnisamehe ili nafsi yangu iweze kutulia. Nina maumivu makali sana ndani ya mtima wangu. Msiponisamehe kwa kweli sitaweza kuishi nikiwa na amani moyoni mwangu. Naombeni tena kwa mara nyingine mnisamehe,” akasema Jully akiwa bado amepiga magoti chini.

“Simama Jully,” akasema Chris lakini ghafla, Laura akadakia:

“Jully naomba uondoke. Sikutegemea kama ungenifanyia ujinga wa namna hii? Yaani kukuamini kote kule kumbe wewe ndiye uliyetaka kunikwamisha? Ondoka tafadhali,” akasema Laura kwa hasira ya wazi kabisa.

“No! No! No! Laura...usifanye hivyo, tunapaswa kushukuru kwa kuwa ameamua kuwa wazi kwetu, mwache, mwache tafadhali,” akasema Chris.

“Baby huyu hafai. Kwa nini unamtetea? Vipi kama leo hii tusingekuwa tumeoana kwa ajili yake?” akasema Laura.

“Hapana...huyu ni mtu mwema, angekuwa mbaya asingetafuta msamaha. Anayetafuta msamaha maana yake ameelewa alipokosea!” akasema Chris.

Laura alionekana kuanza kuelewa. Akatulia na kumuacha Jully aendelee kuzungumza. Mwisho hakuna aliyeona sababu ya kutomsamehe.

“Jully sisi tumekusamehe kutoka ndani, tunaamini ni shetani tu alikupitia. Kikubwa kwa sababu umekiri kosa na tunashukuru Mungu tumefanikiwa kufunga ndoa yetu. Hayo mengine yameshapita, tuache kama yalivyo, sasa tuangalie yanayofauata.

“Baby tuna mambo mengi muhimu ya kufanya kwa ajili ya ndoa yetu,” akasema Chris akimvutia Laura kwake.

Laura akaenda mzimamzima!

Akajitupa kifuani mwa Chris na kutulia hapo, ni kama hawakumuona Jully aliyekuwa mbele yao. Mabusu yalitembea, wakabembelezana mpaka Laura alipotulia kabisa.

“Usijali dear, yameshaisha sawa mama?”

“Nimekuelewa mpenzi.”

Jully alilipiwa chumba hotelini hapo, siku iliyofuata akasindikizwa hadi uwanja wa ndege, akaondoka kwenda Dar es Salaam, kabla ya kuunganisha katika ndege nyingine hadi Kilimanjaro.

***

Chumba kilikuwa cha kuvutia sana, hali ya hewa ilikuwa tulivu sana chumbani. Manukato mepesi yalikuwa yamesambaa na kufanya harufu ya chumba hicho kuwa yenye kuvutia sana.

Laura alionekana mwanamke mpya kabisa mbele ya Chris. Alimwangalia mke wake, akatabasamu. Alikuwa anang’aa. Akamvutia kwake, Laura akatabasamu!

“Mke wangu mpenzi, nakupenda sana. Sitajuta kuwa na wewe daima.”

“Ahsante mume wangu mpenzi, nami nakupenda pia. Wewe ndiye unayekamilisha ndoto zangu. nakupenda sana,” akasema Laura akionyesha kuzidiwa na hisia kali za mahaba.

“Kuna kitu muhimu nataka kukuambia mpenzi,” akasema Chris.

“Niambie baba, ni nini?”

“Unakumbuka nilichokuambia wakati tunakutana Singida?”

“Tuliongea mengi sana baba.”

“Kubwa zaidi.”

“Mh! Sikumbuki.”

“Wewe ni Movie Star.”

“Mh! Kweli dear?”

“Excactilly! Tena tunatakiwa kuingia location haraka sana kuanza sinema yetu. Tunaanza mazoezi Singida wiki ijayo.”

“Tayari unayo stori mpenzi?”

“Haya maisha yetu tu, yanatosha kuwa stori. Ni kisa cha aina yake mpenzi. Nitaanza kuandika script kesho, keshokutwa twende Singida tukamalizie honeymoon, huko tutakuwa kambini kabisa.

“Nataka nikufue kwa wiki mbili nzima, baada ya hapo tutakwenda Dar kuchukua wasanii wengine kisha tutarudi tena Singida kuanza kurekodi.”

“Unalo jina la filamu tayari?”

“Singidani.”

Wote wakacheka.

Laura akamrukia Chris. Bila kupoteza muda, Chris alimtupia kitandani, kisha akazima taa. Kazi ya kutafuta mtoto wa kwanza, ikaanza!

***

“Oke! Kaa tayari...action!” akasema Chris akimwangalia Laura wakati akimfanyisha mazoezi ya uigizaji.

Alikuwa akimfundisha kucheza na hisia na kuvaa uhusika. Hapo walikuwa katika Hoteli ya Katala Beach ‘KBH’ iliyokuwa katika ufukwe wa Singidani mjini Singida.

Kama mzaha, lakini kumbe Laura alikuwa na kipaji cha kuigiza kilichojificha. Walifurahia maisha hotelini hapo, kisha wakarudi Dar kupanga watu wa kuigiza katika Filamu ya Singidani.

Ilikuwa sinema yenye wahusika wakubwa wanne; Dk. Chris, Ramsey, Rose Ndauka na Wema Sepetu. Mastaa hao na wasanii wengine walikaa kambini mwezi mzima wakirekodi.

Laura sasa akawa staa wa filamu za Kibongo. Kazi ambayo ilimpa jina, heshima na mume bora.



Mwisho.

No comments

Powered by Blogger.