Simulizi : Singidani Sehemu Ya Kwanza (1)

Simulizi ya singidani
CHRIS hakuweza kuvumilia zaidi, akatembea kwa haraka akitetemeka miguu. Alipowafikia akasimama na kuwaangalia kwa kuwakazia macho. Si Davis wala Pamela walioshtuka.

Ni kama hawakuona chochote wala yeyote. Wakaendelea na shughuli zao. Muda huohuo, kwa ghafla sana, Chris akasikia kibao cha nguvu mgongoni mwake...

“Nani?” akasema akipaza sauti.

“Cut...” Director Mushi akasema akiwaamrisha wasitishe kuigiza.

Chris akiwa amefura akageuza uso wake. Hamad! Alikutana na uso wa baba yake mzazi ukiwa umekunjamana!

Mzee Joseph Shila.

“Kweli unaweza kuzaa watoto lakini si wote watakuwa watoto bora. Daktari mzima, tena niliyepoteza mamilioni yangu kukusomesha nje ya nchi, unakaa na hawa wajinga wamevaa vichupi mnaigiza?

“Hivi Christopher mwanangu utakua lini wewe? Lini utakuwa mtu mzima na kuelewa ninayokuambia? Pumbaaf, endelea na ujinga wako,” akasema mzee Shila kisha akaondoka zake.

Chris akabaki ameduwaa.

Mushi alibaki anashangaa tu asijue cha kufanya. Neno moja likamponyoka kwa haraka: “What is going on Chris?”

Chris hakujibu.

“Kwa nini tunaharibiana kazi? Hivi kweli scene moja inaweza kutuchukulia siku nzima? Jana ulisema unaumwa kichwa, leo umechelewa location ukasema ulikuwa kwenye upasuaji, baadaye tena sijui unamwita mtu aje kutuharibia kazi ili iweje?

“Kama unaona hutaki kufanya hii sinema si uache kaka? Unadhani wewe ni staa sana siyo? Ni bora kufanya kazi na chipukizi wenye nidhamu kuliko kuhangaika na nyie mastaa mnaotusumbua vichwa kila siku,” akasema Mushi kwa hasira.

Scene hiyo ilimsumbua sana kutokana na ugumu wake...tena siku hiyo walipatia kwa kiasi kikubwa sana kuvaa uhalisia katika kiwango cha juu. Kosa la mzee Shila lilimuumiza sana, maana liliwatoa wasanii katika mwendelezo mzuri wa kuvutia.

“Samahani kaka, unanifikiria vibaya. Yule ni baba yangu.”

“Baba yako?” akauliza Mushi kwa sauti ya upole.

“Ndiyo...ni baba yangu.”

“Imekuwaje?”

“Ni habari ndefu.”

“Samahani sana kaka.”

“Usijali.”

“Upo kwenye mood nzuri na tunaweza kuendelea?” akauliza Mushi.

“Bila shaka.”

“Kweli?”

“Nitajitahidi...”

“Sawa...usijali, tutaendelea palepale...kaeni tayari...kamera upo sawa? Boom please...light...Ok! Action...” akasema Mushi.

“Pamela!!!” neno hilo likamtoka Chris huku machozi yakimiminika kwa kasi sana.

Ilikuwa sauti iliyojaa huzuni na kitetemeshi cha hali ya juu. Kweli alivaa uhusika sawasawa. Ni kweli, tukio lile alitakiwa kutoa machozi, alipaswa kuonyesha huzuni kama alivyofanya.

Hakuna aliyejua ila ukweli ni kwamba alifanikiwa zaidi kutokana na machungu ya kero za mzee wake na si kwa sababu ya tukio lililokuwa ndani ya scene ile.

***

Mzigo mzito ulimjaa Chris kichwani. Mwanamke yule mrembo aliuteka mtima wake. Alikuwa mweusi, mrefu wa wastani mwenye umbo namba nane. Alisuka nywele zake katika mtindo wa rasta nene.

Alivaa sketi fupi ya khaki, iliyofanya miguu yake ya bia ionekane vizuri zaidi. Chris akasahau mawazo yote, akatembea hadi kwenye mlango wa kuingilia chooni na kusimama hapo.

Dakika mbili baadaye yule mrembo alitoka msalani na kumpita Chris pale alipokuwa amesimama. Yule msichana alimwangalia Chris ambaye alijitahidi kutabasamu lakini hakuonyesha kama alimuona! Akapita na hamsini zake. Chris akakasirika!

Na umaarufu wote huo?

Tanzania nzima ilimfahamu kutokana na umaarufu wake kwenye filamu za Kibongo. Mara zote amekuwa mstaarabu na kamwe huwa hatumii umaarufu wake kuwapata wasichana lakini safari hii alitamani sana kutumia silaha hiyo.

Jambo la kusikitisha ni kwamba, silaha hiyo ni kama ilikuwa butu au haiwezi kabisa kutumika. Pengine ingeweza kutumika na ilikuwa na nguvu mujarabu lakini siyo kwa msichana yule!



MARA kadhaa watu walikuwa wakimwangalia na kumnyooshea vidole wakisemezana ndani ya ukumbi huo. Wengine walimfuata na kumsalimia huku wengine wakitaka hata kupiga naye picha tu.

Kwa msichana huyu ni tofauti. Hana muda naye kabisa. Pengine silaha ya kwanza haikuwa na nguvu au msichana yule si mpenzi wa filamu kwa hiyo hamfahamu.

Labda! CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Bado alikuwa na silaha nyingine. Mavazi ya gharama aliyokuwa amevaa yalikuwa ni silaha kwa msichana yeyote wa mjini. Chris alikuwa amependeza sana. Alivaa kawaida tu, lakini alipendeza vilivyo.

Silaha hiyo nayo imeshindikana!

Chris akabaki akimsindikiza kwa macho mpaka alipoishilia. Akaanza kupiga hatua za taratibu kurudi alipokuwa amekaa awali. Lengo likiwa ni kuendelea na mawazo yake yaleyale!

***

Macho ya Chris ni kama yalizingirwa na ukungu. Akaamua kuyapekecha kidogo ili kuuondoa ili aweze kuangalia vizuri. Kweli kabisa...alichokiona ni sahihi.

Ni yule msichana alikuwa anacheza na kundi la vijana watano. Wale vijana walikuwa wamemzunguka, yeye akawa katikati yao. Kuna wakati, walianza kuingia katikati mmojammoja na kucheza na yule mrembo kwa zamu.

Lilikuwa onesho la bure lililovutia ambalo lilisababisha wengine waache kucheza, wabaki kuwaangalia wao. Chris akafura!

“Yaani wale watoto ndiyo wanaweza kushindana na mimi? Haiwezekani. Mimi ni mtoto wa mjini...” akawaza Chris akiinuka kusogea karibu na lile duara la vijana watano wakicheza na msichana yule mrembo!

Yule anayeusumbua moyo wake.

Mtikisiko wa moyo ulimvaa Chris. Hasira zikamkaba rohoni. Aliumizwa na msichana yule mrembo ambaye alikataa hata kumsalimia tu wakati tayari alikuwa ameshaufanya moyo wake mateka. Hasira zake sasa zilihamia kwa wale vijana.

Chris akajikaza na kusimama kisha akasogea karibu na wale vijana. Akatoa macho. Hata yeye alijishangaa ni kwa nini alikuwa na hasira kiasi kile.

Yule msichana hakuwahi kumfahamu kabla na hakuwa mpenzi wake. Kwa nini achanganyikiwe? Labda ni mapenzi, lakini kwa nini awakasirikie watu wengine ambao hawafahamu?

Alikiri moyoni mwake kwamba alifanya makosa.

“Nakosea sasa...nadhani huu umaarufu wangu unataka kunidanganya. Natakiwa kuwa mpole kwanza...” akawaza.

Kitu alichogundua kwa haraka ni kwamba alitakiwa kupata liwazo kidogo. Ingekuwa rahisi zaidi kuliwazwa na msichana yule lakini kwa sababu anajifanya anamkataa, Chris alikuwa na kitulizo kingine.

Alichepuka haraka hadi kwenye kaunta ndogo ya pembeni katika ukumbi ule. Akamvaa msichana aliyekuwa akihudumia.

“Nataka toti tatu za Grant’s haraka tafadhali,” akasema Chris akiweka noti moja ya elfu kumi mezani.

“Kaka Chris hata salamu?” yule mrembo akamwambia.

Chris akageuza uso, akakutana na msichana mrembo, mweupe, mrefu, mwenye macho makubwa ya kung’ara. Alijilaumu sana.

“Wakati mwingine unaweza kupoteza cast hivihivi...huyu msichana anafaa kuigiza,” akawaza akitabasamu.

“Habari yako dada yangu?”

“Salama, sasa mambo si hayo? Kwani ulivyonisalimia umekufa?”

Chris akacheka.

“Wewe utakuwa unatoka katika makabila mawili tu ya hapa Singida, kama siyo Mnyaturu utakuwa Mnyisanzu.”

“Mh! Wewe umejuaje? Mimi Mnyaturu.”

“Umeona sasa! Nilisema tu, nimefurahi kuwa mtabiri mzuri,” alisema Chris huku akiondoka zake.

Anarudi kulekule! Msichana hana jipya kwake, anamtaka yule ya mwanzo. Kadiri muda unavyozidi kwenda anazidi kuwaza tofauti. Si kwamba alimtaka msichana yule kwa usiku mmoja tu; aliwaza ndoa kabisa.

Ilikuwa mapema sana kwake kuanza kuwaza mambo makubwa kama yale lakini ndicho kilichokuwa kichwani mwake. Potelea mbali, hata kama akigombana na baba yake mzee Shila, bora aishi na yule mrembo!

“Nimeshajua cha kufanya!” akajisemea Chris akipiga funda moja dogo, akachanganya na mate, akameza.



SASA alipata wazo jipya. Wazo ambalo kwa hakika lingeweza kumsaidia kumpata yule msichana. Alianza kumfuatilia kijana mmoja ambaye alionekana kama wangeweza kuelewana kidogo. Aliachana na wote, akabaki akimwangalia huyo tu. Mara yule kijana akajitoa pale na kutembea akielekea chumba maalum cha kuvutia sigara. Chris na glasi yake, akamfuata yule kijana.

“Oyaa mambo vipi?” Chris akamsalimia.

“Aaaaah! Mkubwa, bora nimekuona nitapona. Inakuwaje mwana?”

“Salama.”

“Umeingia lini Singapore?”

“Jioni ya leo...samahani huu ni mguu wako lakini kama hutajali kachukue kwanza kinywaji. Unakunywa nini?”

“Ngumu bro.”

“Ngumu?”

“Ndiyo.”

“Unamaanisha nini?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Kitu cha konya ndo mzuka.”

“Sawa, kachukue kubwa na pakiti nzima ya fegi,” akasema Chris akimkabidhi noti mbili za elfu kumikumi.

Yule jamaa akaondoka na dakika mbili tu baadaye alirudi akiwa na chupa kubwa ya pombe kali aina ya konya na pakiti ya sigara. Akamrudishia chenji Chris ambaye alimshika mkono na kumtoa katika kile chumba cha kuvutia sigara.

“Vipi?”

“Njoo huku.”

Waliishia kwenye sofa kubwa ndani ya ukumbi ule, pembeni na meza ya Pool Table ambapo bila kupoteza muda, Chris alianza kumwuliza kuhusu yule msichana.

“Nimewaona muda mrefu mkicheza na yule dada. Vipi unamfahamu vizuri?” akauliza Chris.

“Tunasoma naye.”

“Kati yenu pale kuna mtu wake?”

“Mtu wa wapi? Yule msichana ni mwanafunzi mwenzetu tu, hakuna mwenye kisu kikali pale kaka. Yule demu ni mkali chuo kizima.”

“Mnasoma chuo gani?”

“Uhasibu.”

“Oke! Sikia nikuambie mdogo wangu, yule mtoto mimi nimempenda..siyo kwamba nakuambia kwakuwa sijui kutongoza laah! Nataka tu unisaidie kunikutanisha naye, maana naona kama ananata fulani hivi...mambo mengine nitajua mwenyewe.”

“Usiogope mwanajeshi wangu, hilo limepita.”

“Kweli?”

“Wewe sema unataka aje sasa hivi?”

“Ndiyo...”

“Nakuja naye.”

“Sawa.”

“Njoo kwanza....” Chris akamwita yule kijana ambapo mara moja alirudi.

“Hujaniambia jina lako bado.”

“Naitwa Julius.”

“Poa.”

Julius akaondoka. Kama mchezo hivi, dakika moja baadaye, alifika alipokuwa amekaa Chris akiwa amemshika mkono yule msichana. Akamkalisha kwenye sofa kubwa, akamuweka katikati. Pembeni wakamzunguka na Chris.

“Huyu ni kaka yangu...anaitwa Chris. Nimesoma na mdogo wake JK Nyerere Sekondari, Moshi. Tunaheshimiana sana lakini nimechukizwa na tabia yako ya dharau kwake,” Julius akamwambia yule msichana huku akimkazia macho.

Chris akashtuka.

“Mbona huyu dogo anataka kuharibu sasa?” akawaza.

“Nimemfanyaje?” yule msichana akauliza.

“Hujui? Najua unanata na una dharau lakini kwani wewe humfahamu Chris? Utakuja kupoteza bahati bure wewe mtoto wa kike...si kila mwanaume ni mhuni,” akasema Julius kwa hasira.

Pamoja na kwamba kile alichokuwa akikifanya ilikuwa ni maigizo tu ili kumuunganisha na Chris lakini pia pombe aliyokunywa ilikuwa inafanya kazi yake sawasawa.

“Samahani bro Jully.”

“Siyo mimi, wa kumuomba msamaha ni huyu hapa...mimi nawaacha, naamini utafanya hivyo.”

Yule msichana akatingisha kichwa kukubaliana naye. Julius akasimama na kurudi zake ‘Smoking Room’.

Yule msichana alitulia kwa muda, Chris bila kupoteza muda, akamsogelea kidogo. Naye akaanza kumwangalia kwa macho yanayozungumza. Chris alikuwa akifikisha ujumbe wake moja kwa moja.


INAENDELEA

No comments

Powered by Blogger.