Chombezo : Kivuruge Wa Tandale Sehemu Ya Ishirini na tano (25). MWISHOOO

hadithi nzuri ya kivuruge wa tandale
Nilijikakamua na kugeuka pembeni, nikaona kuna vitanda vingine kibao huku kukiwa na wagonjwa, nikageuka upande mwingine nako nikaona hivyohivyo, ni kweli nilikuwa hospitali.

“Dokta! Amezinduka,” nilisikia sauti ya nesi akimuita daktari. Kumbe kulikuwa na nesi amekaa pembeni ya kitanda changu upande wa miguuni akifuatilia kila kitu nilichokuwa nakifanya. Muda mfupi baadaye, kitanda changu kilikuwa kimezungukwa na daktari na manesi kadhaa.

“Unajisikiaje kijana.”

“Najisikia vizuri ila kichwa kinanigonga, hapa ni wapi na nimefikaje?”

“Hapa ni hospitali, umeletwa baada ya kudondoka na kupoteza fahamu,” alisema daktari huku akinipimapima kwa kutumia kifaa maalum, nikashangaa anawaambia wale manesi watupishe ana jambo la kuzungumza na mimi.

“Kijana umeoa?”

“Hapana dokta, kwa nini?”

“Kuna mama mmoja kati ya wanawake waliokuleta anasema yeye ni mkeo, ili nikikutazama mwili wako na umri wako naona kama hamuendani naye kabisa.”

“Dokta, kwani kushauri mambo ya mahusiano ya kimapenzi ya wagonjwa wako nayo ni miongoni mwa kazi zako?

“Nilimuuliza kijeuri maana niliona anaanza kuniingia mwilini.”

“Siyo hivyo kijana, inaonekana wewe huumwi chochote kwa sababu tumekupima vipimo vyote lakini kuna kitu mimi nataka kuzungumza na wewe kama mwanaume mwenzangu,” alisema dokta kwa sauti ya chini kidogo huku akitazama huku na kule kuhakikisha kama hakuna mtu anayetusikia.

“Hivi huwa unafanya mapenzi mara ngapi kwa kutwa nzima na unakutana na wanawake wangapi kwa siku?”

“Swali gani hilo dokta?” nilimjibu huku nikigeukia pembeni. Nilijua na yeye anataka kuanza kuleta za kuleta kama yule daktari wa Mwananyamala.

“Dalili zote ulizonazo zinaonesha kwamba wewe unafanya ngono sana, hata ulipofikishwa hapa nilipokuchunguza kwa makini niligundua kwamba kuna uwezekano mkubwa ukawa umepoteza fahamu wakati wa tendo, kweli si kweli,” alisema yule daktari huku akinilazimisha nimgeukie.

Sikumjibu kitu, akaendelea kunieleza kwamba kutokana na tabia yangu hiyo, majimaji kwenye viungio vya mifupa (joints) kama kwenye magoti, kwenye mabega, kwenye kiuno na sehemu nyingine zenye viungio yalikuwa yamekauka.

Aliniambia pia kwamba nilikuwa na upungufu mkubwa wa maji na damu ambavyo vyote ni kwa sababu ya kuushughulisha sana mwili kwa kufanya mapenzi. Aliniambia kitaalamu, kufanya tendo la ndoa, unapopiga mshindo mmoja, nguvu inayotumika ni sawa na kutembea kwa miguu kwa kilometa kibao.

“Hapana dokta, naona sasa unaleta stori za vijiweni,” nilimkatisha kwa sababu vijiweni huwa kuna stori nyingi za aina hiyo, mwingine anakwambia kupiga mshindo mmoja ni sawa na kutembea 3 kwa miguu, mwingine anakwambia ni sawasawa na kilometa saba na kadhalika.

Kama ungefuata stori hizo za vijiweni, maana yake ni kwamba kwa muda wa wiki moja tu mimi ningekuwa nimeshapita Morogoro na sasa naitafuta Dodoma kwa miguu kwa sababu nilikuwa nimefanya sana, tena kwa wanawake tofautitofauti.

“Sawa, zinaweza kuwa ni stori za vijiweni lakini hoja ya msingi unayotakiwa kuijua hapa, ni kwamba unapofanya tendo la ndoa, nguvu unayotumia kwa kila mshindo ni kubwa sana kwa hiyo unapofanya hovyohovyo siyo kwamba unaonesha uhodari wako, bali unaumaliza kabisa mwili wako.

“Tazama ulivyokonda, kiuno kimebaki kama nyigu, hujionei huruma?”

“Hizo sasa dharau dokta, kama unaweza kunitibu wewe nitibu lakini siyo kunisimanga kwa sababu hata kiapo cha kidaktari sidhani kama kinakufundisha kumsimanga mgonjwa.”

“Yapo magonjwa ambayo mtu unaweza kumuonea huruma mgonjwa, lakini siyo mambo ya kishenzi kama yako, angalia dripu inavyoingia kwa kasi kwenye mwili wako, umekaukiwa kabisa maji. Unawaona hawa wagonjwa wengine, kila mmoja anaumwa sana lakini hakuna aliyejitakia kama wewe.

“Lile limama kubwa namna ile eti linasema wewe ndiyo mume wake, si lazima litakuwa linakutumikisha kingono? Acha uboya wewe,” alisema daktari huku akiondoka, akionesha kukasirika.

Hii ilikuwa mara ya pili sasa nakutana na suala kama hilo, mara ya kwanza ilikuwa ni kule Mwananyamala na yule daktari baada ya kunisemea mbovu, nilihisi ni kwa sababu ya wivu kwani nilikuwa na Khazija, lakini huyu naye ambaye kiumri alikuwa mkubwa kidogo, naye alikuwa akizungumza maneno yaleyale.

Niliona sasa kuna haja kweli ya kuyafanyia kazi yale waliyoniambia kwa sababu ilionesha kabisa kwamba nikiendelea na mchezo huo, siku zangu zinahesabika. Dakika chache baadaye yule daktari alirudi tena pale kitandani kwangu, akaendelea kunichana wakati mwingine akitumia maneno ya kuudhi.

“Wewe bado ni kijana mdogo sana, kwa nini usitafute mwanamke mnayelingana naye, ukafuata taratibu zote zinazotakiwa ili awe mkeo halali badala yake una kazi ya kuparamia watu wazima?”

“Dokta, hebu naomba uniache tafadhali, nimekusikia.”

“Wewe jifanye kichwa ngumu, siku nyingine ukiletwa hapa hata kama unakaribia kupoteza maisha, tutakuacha maana inaonekana wewe mwenyewe hujijali.”

“Tusifike huko dokta, unajua mimi ni kama ndugu yako,” nilijirudi baada ya daktari kuanza kutoa maneno makali, alionesha kweli kukasirishwa na kilichotokea.

Nilipoonesha kukubali makosa, na yeye alipunguza jazba na kuniambia madhara ya kiafya ya kufanya ngono hovyo na watu tofautitofauti, huku akinionya kwamba ukiachilia mbali mateso niliyokuwa nayapata, naweza pia kuambukizwa magonjwa ya zinaa, ikiwemo Ukimwi.

Alinipa elimu kubwa sana ambayo siyo kwamba sikuwa naijua kwa sababu hata yule daktari wa Mwananyamala alishanieleza, moyoni nikajiapiza kwamba nitafanya kila kinachowezekana ili kuondokana na hatari iliyokuwa mbele yangu.

Basi niliendelea kupewa matibabu pale na muda wa kuona wagonjwa ulipofika, kizaazaa kikubwa kiliibuka wodini kwani ukiachilia mbali Madam Bella ambaye ndiye aliyenileta pale hospitali, lakini pia alikuwepo Salma ambaye ndiye aliyenizimisha, alikuwepo Khazija wangu ambaye alishapewa taarifa lakini naye alikuja na mama mwenye nyumba, Ruqaiya naye sijui alipewa taarifa na nani kwani naye alikuja akiwa na mapochopocho kibao kwa ajili ya mgonjwa, sambamba na Nancy, ambaye sijui aliambiwa na nani.

Nikawa nimezungukwa pale kitandani na wanawake zangu wote, ambao kila mmoja alikuwa ameleta chakula na kila mmoja alikuwa anataka wenzake wamtambue kwamba yeye ndiye mpenzi wangu.


Nilichokifanya, niliamua kutengeneza bonge la ‘script’ kama wasanii wa Bongo Muvi kwa sababu nilijua muda wowote kinaweza kunuka.

Nikajifanya kama najisikia maumivu makali sana, nikamuagiza Ruqaiya akamuite daktari, akaweka kikapu chake chini na kutoka mbiombio kuelekea kule kwenye ofisi ya nikamuagiza Khazija akaninunulie maji ya moto nje, nikamuagiza pia mama mwenye nyumba akanitafutie dawa ya kupunguza maumivu.

Niliwachanganya wote kwa makusudi kwa sababu sikutaka waendelee kukaa pamoja nikiamini lazima kuna jambo baya litatokea na kuwa skendo pale hospitalini. Kweli dili lilitiki, wote wakasambaratika na kuniacha peke yangu pale kitandani.

Muda mfupi baadaye, Khazija alirudi akiwa ameongozana na yule daktari aliyekuwa akinitibu, akaniinamia kwani nilikuwa naugulia kwelikweli.

“Unajisikiaje?”

“Dokta, wewe ni mwanaume mwenzangu, naomba unisaidie tafadhali.”

“Dada, hebu naomba utupishe kidogo,” alisema dokta akimwambia Khazija, kweli akatii na kusogea pembeni maana nilivyokuwa nazungumza naye, nilikuwa nataka mtu mwingine yeyote asijue kinachoendelea.

“Hawa wanawake wote ni wanawake zangu.”

“Unasema?”

“Ndiyo dokta, sasa hapa wanaweza kusababisha matatizo zaidi.”

“Mkeo halali kati ya hawa ni yupi?”

“Yule aliyekuja kukuita ndiyo mimi nina malengo naye, wale wengine si unaona kwanza wengine ni watu wazima?”

“Unawezaje kuwa na wanawake wakubwa na wengi kiasi hiki?”

“Dokta nisaidie.”

“Nakusaidia nini sasa?”

“Naomba uwazuie wasiingie tena wodini na kama wakiingia, waje mmojammoja, ikiwezekana waambie kabisa kwamba umenipima na kunikuta na Virusi vya Ukimwi,” nilisema, akashtuka na kunitazama:

“Umechanganyikiwa nini kijana?”

“Hapana dokta, nisaidie.”

“Miiko ya kidaktari hairuhusu kabisa kufanya hicho unachokitaka, tafadhali tusiharibiane kazi.”

“Dokta! Dokta,” nilisema huku machozi yakianza kunilengalenga. Alinitazama kwa huruma kwani kiukweli nilikuwa na hali mbaya, ukiachana na sekeseke hilo la wanawake hao, bado afya yangu haikuwa nzuri kabisa na nilihitaji msaada.

“Siwezi kuwazuia kuja kukuona kwa muda huu kwa sababu ni muda wa kutazama wagonjwa, ninachoweza kukifanya ni kuzuga hapa kama naendelea kukuhudumia mpaka muda wa kuona wagonjwa utakapoisha,” alisema, nikatingisha kichwa kukubaliana naye.

Basi alijifanya kama ananipimapima huku na kule, mara arekebishe dripu, mara anipime mapigo ya moyo, ilimradi tu aonekane yupo bize.

Wale niliowazuga, wote tayari walikuwa wamesharejea, huyu akiwa na chupa ya maji, mwingine akiwa na vocha, na mwingine akiwa na matunda, basi na mimi nikawa nazidi kugugumia kama naumia sana.

“Inabidi nikuhamishie wodi ya private, utaweza kulipia?”

“Nina bima kubwa dokta, we nihamishe tu dokta,” nilimwambia. Kweli akawaita manesi na kuwaelekeza kunihamisha harakaharaka, na mimi nikawa nazidi kujilegeza ili hali yangu ionekane kuwa mbaya.

“Samahani, nyie ni ndugu wa huyu mgonjwa?” nilimsikia yule daktari akiwauliza, wote wakajibu harakaharaka huku kila mmoja akimsogelea mwilini ili ionekane yeye ndiyo yupo karibu na mimi.

“Kwa nini hamumsimamii mgonjwa anywe dawa zake za kurefusha maisha mnasababisha anazidiwa kama hivi?”

“Mungu wangu?” wote walisema kwa pamoja utafikiri walioambizana, daktari akaanza kuwasema kwamba wao ni ndugu gani wasiojali afya yangu kiasi cha kushindwa kunisimamia ninywe vidonge vyangu vya ARV?

“Dokta, kwani vidonge vya ARV si wanakunywa wenye maambukizi ya Virusi vya Ukimwi?”

“Ndiyo! Kwani nyie hamna taarifa kwamba huyu ndugu yenu ni mwathirika? Eti, au hukuwaambia ndugu zako?” Dokta aligeuka na kuniuliza, muda huo tayari manesi wakiwa wameshaanza kukisukuma kitanda changu kuelekea wodi ya wagonjwa binafsi.

Moyoni nilitamani kucheka kwa jinsi walivyopatwa na mshtuko kusikia maneno hayo kwa sababu ni kweli wote walikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mimi na hakuna hata mmoja kati yao ambaye tulifanya mapenzi kwa kutumia kinga.

Nadhani moyoni mwao kila mmoja akawa anajisemea ‘nimeshaambukizwa ngoma’. Sikuwajali kwa sababu moyoni nilikuwa najua kwamba nafanya hivyo kwa sababu gani.

“Nani mke wa huyu mgonjwa kati yenu?” dokta aliuliza huku akitembea harakaharaka kunifuata kule nilikokuwa napelekwa. Sikuwa mbali kwa hiyo niliweza kusikia kila kilichokuwa kikizungumzwa, nikaona wote wakikwepa kwa kasi swali hilo.

“Mimi ndiyo mkewe,” alisema Khazija, sijui alipata wapi ujasiri huo lakini nadhani ni kwa sababu na yeye alishapima, tena siku chache zilizopita kwa hiyo alikuwa na uhakika kwamba mimi na yeye tupo salama.

“Basi wewe mkewe ndiye utakayeruhusiwa kuingia humu wodini, wengine jamani naomba mnisubiri nimhudumie mgonjwa naona virusi vyake vimechachamaa,” alisema daktari, akafunga mlango kwa ndani.

Kiukweli nilikuwa najizuia sana kucheka japokuwa nilikuwa naumwa, Ukimwi usikieni tu lakini kiukweli unatisha sana. Basi hata sijui kila mmoja aliondoka saa ngapi lakini daktari alipokuja kutoka, hakuna aliyekuwepo pale nje ya wodi niliyokuwa nimelazwa.

“Jamani mume wangu, mbona hujipendi kiasi hicho? Yaani hawa wote ni wanawake zako?”

“Hapana, walikuwa wanawake zangu zamani, tena kwa nyakati tofauti, sina taimu nao tena.”

“Muongo mkubwa wewe, hawa wengine mbona nawafahamu kabisa na nimewafahamia kwako?” Khazija alianza kulalama tena. Ikabidi nimpe ‘option’ moja muhimu, nikamwambia nikipona nataka tuhame kabisa mji, ikiwezekana twende Arusha au kwao Zanzibar, tubadilishe namba za simu na kukata mawasiliano kabisa ili tuanze maisha mapya.

Alifurahi sana na akanihakikishia kwamba wazazi wake wanao uwezo mkubwa wa kutusaidia kama tukiamua kwenda kuishi Zanzibar, ila akanisisitiza ni lazima nimuoe tuwe mume na mke kama tulivyokubaliana.

Basi niliendelea kutibiwa na baadaye nikapata ahueni, tukaruhusiwa kurudi nyumbani lakini kwa sababu maalum, tulienda kulala hotelini na Khazija. Usiku huo tukanunua laini nyingine za simu na kabla sijatoa ile laini yangu inayofahamika, niliwatumia meseji wote kuwaaga kwa sababu sikuwa naachana nao kwa ubaya.

Nikawaambia wasiwe na wasiwasi kwa sababu mimi sina Ukimwi kama daktari alivyosema, nikawataka kila mmoja kwa wakati wake aende hospitali kuhakikisha ila nikawaambia kwamba nimeamua kuoa na kutulia kwa hiyo nahama mji. Nikazima simu muda huohuo na kutoa laini, nikaivunjavunja na kuweka ile nyingine.

Kesho yake asubuhi tulienda mpaka bandarini, tukakwea boti na safari ya kuelekea Zanzibar na Khazija ikaanza. Miezi michache baadaye, afya yangu ikiwa imeimarika kabisa, nikiwa pia nimepata ajira kama mtaalamu wa teknolojia ya mawasiliano kwenye hoteli iliyokuwa inamilikiwa na baba yake Khazija, nilifunga rasmi ndoa na Khazija na kuwa mke wangu wa halali na huo ukawa mwisho wa tabia yangu ya ukivuruge.


Mwisho. .

No comments

Powered by Blogger.