Simulizi : Singidani Sehemu Ya Kumi na Tatu (13)

Simulizi ya singidani
CHRIS alichanganyikiwa sana, alimwangalia baba yake akiwa haamini kabisa kama tayari alikuwa ameshajua kila kinachoendelea. Alihisi kichwa kumuuma sana.

Alibaki amesimama palepale akimwangalia baba yake. Ndoa yake na Laura ilikuwa inayeyuka, jambo ambalo hakutaka kabisa litokee.

“Una jipya la kuniambia?” Mzee Shila akauliza kwa hasira.

“Baba tuliza hasira kwanza. Nahitaji kuzungumza na wewe.”

“Sitaki mazungumzo na wewe, naomba uondoke haraka sana mbele ya macho yangu. Toka tafadhali,” akasema mzee Shila kwa hasira.

Chris hakuwa na cha kufanya zaidi ya kuondoka. Baba yake alikuwa amekasirika katika kiwango cha mwisho kabisa. Aliingia garini kisha akapiga gia hadi nyumbani kwake Kijitonyama.

Alifikia sebuleni na kujitupa kwenye sofa kubwa, akijaribu kutafakari. Macho yake tayari yalishaanza kulengwalengwa na machozi. Bila hiyari yake akajikuta akianza kulia.

Hakuwa na msaada wowote kwa wakati ule. Alisimama ghafla na kuelekea kwenye jokofu kisha akatoa bia moja na kuifungua, akiwa palepale mbele ya jokofu lake, aliimimina kinywani mwake yote ikaishia humo!

Aliposhusha chupa, ilikuwa tupu kabisa. Akachukua bia nyingine, akafanya vilevile kisha akachukua tena ya tatu, safari hii akatembea hadi kwenye sofa na kuketi.

Akaendelea kunywa!

Ni kama alikuwa amechanganyikiwa kabisa. Jambo lile lilimuumiza sana na aliona kama dunia yote ilikuwa ikimuangukia yeye.

Amkose Laura?CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Ni jambo ambalo hakutaka kabisa kuliruhusu litokee. Alihisi mwili wote ukitetemeka. Akiwa katika hali ile, akapata wazo la ghafla. Aliona usalama wake ulikuwa kwa mzee Ngeleja.

Lilikuwa wazo alilolipitisha moja kwa moja. Haraka akachukua simu kisha akabonyeza jina la mzee Ngeleja na kumpigia! Simu haikuita muda mrefu, tayari mzee Ngeleja alikuwa hewani!

“Shikamoo baba,” Chris akasalimia kwa heshima.

“Marahaba mwanangu, vipi mnaendeleaje na maandalizi huko?”

“Mambo yameharibika.”

“Kuna nini? Hebu niambie mwanangu, acha kuniweka roho juu mimi na huu utu uzima.”

“Baba amegundua kila kitu. Amejua mchezo wote. Amefahamu kuwa Laura siyo Mnyiramba. Hataki kusikia ndoa tena, amesema ataongozana na mimi hadi kijijini akanitafutie mke yeye mwenyewe!” Akasema Chris huku akilia.

Kimya cha sekunde kadhaa kilipita. Mzee Ngeleja alibaki kimya huku sauti ya kilio cha Chris ikisikika kwenye simu. Baadaye mzee Ngeleja akaanza tena kuzungumza...

“Mwanangu kwanza nataka kukuambia, ni afadhali jambo hilo limetokea!”

“Afadhali? Kwa nini baba?”

“Ingewasumbua sana baadaye!”

“Kwa hiyo mzee uko tayari kuona ndoa yangu na Laura inayeyuka?”

“Kwanza nataka kukutia moyo mwanangu. Hakuna ndoa inayoyeyuka hapo. Kwanza tayari ninyi ni wanandoa halali, maana mmefunga ya kimila. Hilo ondoa shaka kabisa.

“Jingine ni kwamba, hilo ni jambo dogo sana ambalo lipo ndani ya uwezo wangu. Najua naweza kulishughulikia.”

“Kivipi baba? Utafanyaje wakati wewe uko huko mbali?”

“Kesho nakuja Dar, naomba uwe na amani. Kwa sasa jambo hili lifanye siri kabisa. Usimwambie hata Laura kama kuna kitu kama hicho kimetokea.”

“Sawa baba.”

“Ok! Siku njema, naomba uwe na amani.”

“Ahsante.”

Wakakata simu zao.

Angalau sasa Chris alihisi amani moyoni mwake. Aliendea kunywa akiwa na matumaini ya ndoa yake kufungwa baada ya mzee Ngeleja kuahidi kumsaidia.

***

Saa 10:00 alasiri, mzee Ngeleja akiwa ameongozana na mchungaji wa kanisa lililotarajiwa ndoa ya Laura na Chris kufungwa na mwenyeji wao Chris, walikuwa mbele ya geti la mzee Shila, Mbezi Beach.



Kwa bahati nzuri, mzee Shila mwenyewe alikuwepo ndani. Chris aliwakaribisha na wote wakaingia hadi ndani. Sebuleni walimkuta mzee Shila amekaa na mkewe.



Aliwakaribisha kwa hofu akiwa hajui ni akina nani na walichofuata nyumbani kwake. Kwa utulivu mkubwa, mzee Ngeleja aliketi, kisha mchungaji.

“Karibuni jamani,” akasema mzee Shila akionesha wasiwasi kidogo.



“Ahsante, nafurahi tumewakuta, tena wote kwa pamoja. Labda tujitambulishe, mimi naitwa mzee Ngeleja natokea Mwanza, ni baba mzazi wa Laura ambaye kwa wewe unamfahamu pia kwa jina la Njile, mchumba wake na Chris,” mzee Ngeleja akasema kisha akatulia kidogo.

Mzee Shila akatoa macho, hakuweza kuzuia hasira yake.

“Nimeongozana na mchungaji Samatta, huyu tumempitia mimi na Chris kanisani wakati tunakuja hapa nyumbani,” akasema kwa hekima sana mzee Ngeleja.

“Karibuni sana.”



“Ahsante. Kikubwa ni kuhusu vijana wetu, nimetoka Mwanza kwa ajili ya jambo hilo. Nahitaji tuweke haya mambo sawa!” Akasema mzee Ngeleja.

“Mchungaji nakuheshimu sana, mzee mwenzangu nakuheshimu pia, lakini sijaona mtu wa kubadilisha maamuzi yangu. Nilichoamua nimeamua,” akasema mzee Shila.

“Lakini mume wangu...” akadakia mama Chris.

“Kaa kimya! Wakati wanaume wanazungumza unatakiwa kufunga bakuli lako!” akasema mzee Shila kwa ukali.





MAMA Chris alitulia. Alimjua vizuri sana mumewe na tabia zake. Ni wazi kuwa kama angeendelea kubishana naye, jambo lolote baya lingeweza kutokea, kitu ambacho hakukitaka kabisa.

Mchungaji alimwangalia mzee Shila ambaye uso wake ulijaa makunyanzi kutokana na hasira iliyokuwa imemkolea. Ilikuwa lazima afanye kitu kwa ajili ya kijana Chris ambaye alikuwa na jambo jema tu la kutaka kuoa.



“Mzee Shila, nakubaliana na wewe, lakini nakuomba usitumie maneno makali. Hebu tuzungumze kwa utaratibu ili tuone cha kufanya,” akasema Mchungaji kwa sauti ya kusihi sana.



“Kuna kipi cha kujadili hapa Mchungaji?” akauliza mzee Shila kwa sauti ya chini kidogo.

“Sababu hasa za kukataa kijana wako asimuoe huyo binti, maana maandiko yamefafanua wazi kuwa, mwanamke ataacha familia yake na kuungana na mwanaume, nao watakuwa mwili mmoja. Jambo ambalo vijana wetu wapo tayari kwa hilo.



“Sasa inawezekana kama mzazi ukawa na mawazo mazuri tu au sababu zinazosababisha uzuie, ni vyema basi ukasema mzee Shila,” akasema Mchungaji.



“Kikubwa ni kwamba nataka mwanangu aoe nyumbani kwetu, ndicho nilichomwagiza na alifanya hivyo lakini kumbe alikuwa ananidanganya. Amenifanya maigizo mimi. Mpaka ndoa ya kimila imeshafanyika nikijua ni binti wa nyumbani lakini kumbe haikuwa hivyo,” akasema mzee Shila kwa hasira.

Mchungaji akatulia.



Akamwangalia Chris, kisha akamtupia swali: “Anayosema mzee ni ya kweli?”

“Ndiyo Mchungaji.”

“Kwa nini umefanya hivyo?”



“Nakiri makosa Mchungaji. Unajua kubwa ni kwamba mimi nilikutana na Laura Singida, nikampenda sana. Nikajaribu kumchunguza, nikagundua kuwa ana mapenzi ya kweli kwangu, ndiyo maana nikafanya yote hayo.



“Najua nimekosea lakini namuomba baba anisamehe, ila namhakikishia kwa asilimia kubwa, mwanamke ambaye nataka kuoana naye ana tabia njema, anafaa kuwa mke wangu, hilo namhakikishia baba,” akasema Chris kwa sauti ya upole.“Labda mimi niongezee hapo kidogo,” akasema mzee Ngeleja baada



ya ukimya wa muda mrefu.

Wote wakamgeukia.

“Binti yangu alikuja nyumbani na kuzungumza na mama yake kuhusiana na suala hili. Mke wangu alikataa kabisa. Alikataa binti yake asiolewe na Chris kwa sababu ni msanii wa filamu.



“Alisema wasanii wote ni wahuni, hawana tabia nzuri na hawezi kuwa mwaminifu kwenye ndoa. Mwanangu alishindwa kulala siku hiyo, maana alizungumza na mama usiku usiku akiwa ameingia tu kutokea chuoni Singida.



“Baadaye alifikia uamuzi wa kuja ofisini kwangu kuzungumza nami kuhusu jambo hilo. Nilimsikiliza, hoja za mama yake sikuzidharau lakini kama mzazi nilitakiwa kufanya uchunguzi.

“Nilichofanya, nilimwagiza Laura amwambie Chris aje Mwanza aonane na mimi. Kweli akaja. Nikazungumza naye na kumwuliza maswali. Niseme ukweli, kama mzazi ambaye nimemlea mwanangu kwa maadili, nilivutiwa na Chris.



“Mawazo ya mama yake nikaona hayakuwa na uchunguzi. Nilikubaliana na Chris, akaondoka akiwa hajui kama kuna jambo lolote lililotokea. Nilipofika nyumbani nikazungumza na mwenzangu na nilimweleza yote hayo bila kumficha.

CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Alinielewa lakini baada ya mvutano wa muda mrefu sana. Hata hili lilipotokea huku Dar, Chris alinishirikisha na niliamua kuja ili nizungumze na mzee mwenzangu tuweke haya mambo sawa.



“Nashauri, tuwaache hawa watoto waoane. Tuwape baraka zetu kama wazazi. Wanapendana kwa dhati na nakuhakikishia mzee mwenzangu, binti yangu nimemlea kwa malezi bora,” akasema mzee Ngeleja.

Ukimya ukatanda!



Mzee Shila akavuta pumzi ndefu sana, kisha akazishusha taratibu kabisa. Akamwangalia mwanaye... ni wazi kuwa kuna kitu alitaka kuzungumza...

“Ni kweli ulikwenda Mwanza kuonana na huyu mzee?”

“Ndiyo baba.”



Maneno ya mzee Ngeleja yalimwingia sana. Alionekana dhahiri kutaka kukubaliana naye. Mzee Ngeleja alizungumza maneno ya msingi sana. Ghafla mzee Shila alisimama, akasogea alipokuwa amekaa mwanaye Chris.



Akamwonyesha ishara kuwa asimame. Chris akasimama. Akamvutia kwake na kumkumbatia.

“Mwanangu nimekubaliana na wewe, tuachane na yote yaliyopita...” akasema mzee Shila.

Mama Chris akasimama, mzee Ngeleja akafuata, wote wakaunda duara dogo na kushikana mikono. Mchungaji akaanza maombi!

Kikao kikaisha!

***

Mazungumzo yaliyofuata yalikuwa ya kifamilia zaidi yaliyojaa upendo. Mzee Ngeleja alikaribishwa rasmi nyumbani na alipewa heshima zote. Alikaa hapo hadi jioni kabisa, wakizungumza mipango mbalimbali ya ndoa ya Laura na Chris.



INAENDELEA

No comments

Powered by Blogger.