Simulizi : Singidani Sehemu Ya Kumi na Mbili (12)
Lilikuwa wazo zuri sana, kwa jinsi baba yake alivyozungumza, alionekana wazi kukubaliana naye lakini alitaka kuonana na Chris ili wazungumze na kufahamiana.
“Anaweza baba, hilo halina shida.”
“Sawa, nadhani hili tumemaliza, nenda zungumza naye, mpange siku ya kuja. Iwe mapema kabla hujarejea chuoni Singida.”
“Sawa baba, kazi njema.”
“Ahsante binti yangu.”
Laura akaondoka ofisini kwa baba yake, angalau kichwani akiwa amepunguza mawazo. Sasa alikuwa na mwanga kuwa Chris angeweza kuwa mwanaume wa maisha yake.
***
Aliposhuka chini ya Jengo la Kaijage, kitu cha kwanza Laura kufanya ilikuwa ni kumpigia Chris. Alipiga simu mara moja tu – ikapokelewa.
“Baby vipi?” Laura aliongea.
“Poa, mambo?”
“Safi kabisa.”
“Afadhali umenipigia, nilikuwa nakupigia sasa hivi.”
“Kuna nini tena?”
“Nilitaka unitumie picha zako kwenye WhatsApp. Nilizungumza na wazee kuhusu wewe, wanatamani kukuona japo katika picha tu,” akasema Chris.
“Mh! Haina shida mpenzi wangu, mimi nina kubwa zaidi.”
“Kubwa gani?”
“Ni stori ndefu sana mpenzi lakini kikubwa, baba yangu anataka kuonana na wewe. Nimeongea naye kwa kirefu sana kuhusu mimi na wewe!” akasema Laura.
“Dah! Kwani hukuzungumza na mama?”
“Mama ndiyo amesababisha yote hayo lakini hakuna tatizo, dalili ni nzuri,” akasema Laura.
“Unamaanisha nini?”
“Mama alianza kuleta vikwazo ndiyo maana nikaamua kumwambia baba, hivi tunavyoongea nimetoka ofisini kwake,” akasema Laura kwa sauti ya taratibu kabisa.
Chris alishtuka sana!
Ni Mkristo, sijawahi kuwa na mtoto na sina mke na sijawahi kuoa. Naamini nimejieleza vizuri kiasi mzee wangu, lakini kama utaona kuna kitu nimeacha unaweza kuniuliza,” akasema Chris.
“Ahsante sana, nimekuelewa vizuri Chris, napenda kukuita Dk. Chris. Naomba kwanza uniruhusu!”
“Ndiyo taaluma yangu mzee, ruksa kutumia.”
“Ahsante sana Dk. Chris, kwa hakika unajua kujieleza vizuri sana, nataka kukuambia kwa maelezo yako mafupi, nakuhakikishia kuwa binti yangu umempata!” akasema mzee Ngeleja.
Chris akatabasamu!
SASA ENDELEA...
LAURA naye akafanya hivyo. Kwa furaha Chris alisimama na kunyoosha mkono wake kuelekea kwa mzee Ngeleja. Kitu cha ajabu ni kwamba, mzee huyo hakupokea mkono wake, zaidi akasema...
“Lakini kuna tatizo kidogo Dk. Chris.”
“Tatizo gani?” Chris akauliza haraka akionekana kushtuka sana.
Tayari matumaini ya kumpata Laura yalianza kufutika tena. Kitendo cha mzee Ngeleja ambaye ni kama alikuwa mtetezi wake kusema kuna tatizo kidogo, kulimaanisha kumkwamisha kwenye zoezi lililokuwa mbele yake.
Mzee Ngeleja alibaki kimya!
Chris alikuwa bado amesimama vilevile. Akamwuliza tena: “Kuna tatizo gani mzee wangu?”
“Tuliza moyo Dk. Chris,” akasema mzee Ngeleja akiachia tabasamu mwanana.
“Nimeshtuka sana.”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Lazima iwe hivyo.”
“Lakini ni nini hasa?”
“Naona njia mliyotumia haikuwa sahihi. Kwa nini mliwadanganya wazazi?”
“Unamaanisha kule kijijini?”
“Ndiyo.”
“Kulikuwa hakuna kitu kingine cha kufanya zaidi ya hivyo baba. Kumbuka msimamo wa baba yangu ulikuwa huo; kwamba lazima nioe kijijini. Laura siyo wa kijijini baba, ningefanyaje?”
Mzee Ngeleja akakaa kimya.
“Naomba utusamehe baba, lakini tulilazimika.”
“Tena baba, naomba uwe upande wetu katika hili. Sisi tunajua tunachotengeneza. Lengo letu ni zuri na najua litamfurahisha kila mmoja baadaye. Kwa sababu tumeshalianza kwa mtindo huu, naomba liishe hivyohivyo kwanza,” akadakia Laura.
“Wazo zuri sana Laura,” akasema Chris.
“Kwahiyo mnanishawishi nijiunge nanyi kusema uongo?” mzee Ngeleja akasema kwa hamaki.
“Si kwa maana hiyo baba. Lakini kama tulivyosema lengo letu ni zuri.”
Mzee Ngeleja akatulia tena.
“Sawa. Nimekubaliana nanyi, endeleeni na taratibu nyingine. Mimi kwa upande wetu huku mniachie sawa?”
“Sawa baba.”
“Basi sawa, yangu mimi yalikuwa ni hayo mwanangu Chris. Laura unaweza kumsindikiza mwenzako. Vipi ratiba yako? Utakuwa hapa leo ukiendelea kula sangara na sato au unaondoka leoleo?” akauliza mzee Ngeleja.
“Leo nipo, nina tiketi ya ndege ya kesho jioni maana sikujua mazungumzo yetu yangechukua muda gani.”
“Sawa, Laura msindikize mwenzako ili apate hoteli, maana najua kwa hapa mjini si mwenyeji.”
“Hakika baba, mimi nakwenda, ila nina zawadi yako!” akasema Chris akimkabidhi mzee Ngeleja begi dogo.
“Kuna nini humu?” akasema akitabasamu.
“Utaona ukifungua mwenyewe.”
“Ahsante sana dokta, nashukuru.”
Wakaagana.
**
Ilikuwa siku nyingine mpya kwa Chris na Laura. Waliongozana hadi hotelini ambapo mazunguzo ni kama yalianza upya kabisa. Chris hakuamini kama mambo yangekuwa rahisi kiasi kile hasa baada ya kuambiwa na Laura kuwa kulikuwa na tatizo kwa wazazi wake.
“Siamini dear,” akasema Laura.
“Siamini pia, lakini hapa mambo yanatakiwa kwenda harakaharaka kama ambavyo imepangwa. Mambo mengine yatajulikana baadaye.”
“Sawa baby.”
Chris alicharuka, Laura akasisimka. Ni kama damu zilikuwa zikiwaka moto. Ghafla walirukiana na kukutanisha ndimi zao. Kazi ya kufyonzana ikaanza. Waligalagala kitandani kwa muda mrefu kabla ya habari kuhamia kwenye upande wa kimataifa!
Wote walikuwa na uchu kama ndiyo kwanza walikuwa wamekutana siku hiyo. Jioni kabisa, Laura alirudi nyumbani kwao. Ilikuwa lazima awahi kabla baba yake hajarudi.
Chris alilala akiwa na uhakika wa kuingia kwenye ndoa na mwanamke wa maisha yake. Mwanamke ambaye alijihakikishia kumpenda kwa dhati ya moyo wake.
***
Mzee Ngeleja alirudi nyumbani akiwa na furaha sana. Alizungumza na mkewe chumbani kuhusu Chris na binti yao Laura. Mkewe hakuwa tayari kabisa kumwelewa kwa maelezo yaleyale; wasanii ni wahuni!
“Mke wangu achana na mawazo hayo, mimi nimekutana na Chris na kuzungumza naye.
Mimi ni mtu mzima, naelewa vizuri haya mambo. Yule kijana ni mtu mzuri sana, hana shida na anafaa kabisa kuoana na binti yetu,” akasema mzee Ngeleja.
Mkewe akashtuka!
MAMA Laura hakutegemea kuwa mumewe angeweza kuwa ameshakutana na Chris na kuzungumza naye. Kwake, Chris alikuwa kijana mhuni kwa vile tu alikuwa msanii wa filamu.
Kitendo cha kumwambia kuwa alikutana naye, kilimshangaza sana. Mama Laura alitoa macho na kumwuliza mumewe:
“Umekutana naye wapi?” akauliza kwa hamaki.
“Ofisini kwangu, leo hii amekuja Mwanza na kesho asubuhi anaondoka. Naomba ukubaliane na mimi, maana siwezi kukubali binti yangu akaolewa na kijana mpuuzi!”
Mama Laura akatulia.
Baadaye akasema: “Lakini mume wangu unapaswa kufikiri zaidi kuhusu hili. Naona kama utakuwa umeamua harakaharaka sana.”
“Hapana, mimi ni mtu mzima na nina uelewa mzuri. Najua ninachokifanya,” akasema mzee Ngeleja kwa kujiamini.
Mama Laura alikaa kimya tena. Safari hii utulivu ulikuwa wa hali ya juu zaidi.
Mzee Ngeleja akafungua lile begi na kutoa zawadi alizopewa na Chris. Kulikuwa na mashati mawili ya kitenge, saa, mkanda na tai mbili. Pia kulikuwa na doti tatu za vitenge vya gharama.
“Ona hizi ni zawadi alizotuletea. Ndiyo nafungua muda huu hapa. Chukua na vitenge vyako,” akasema mzee Ngeleja akimkabidhi mkewe.
Taratibu mama Laura akaonekana kuanza kuelewa somo, si kwa sababu ya zawadi bali utii alioanza kuhisi Chris anao.
“Nakubaliana na wewe mume wangu! Nakubali Chris amuoe binti yetu. Nimeanza kuhisi kitu tofauti sasa, bila shaka nimebadili uamuzi wangu.”
“Ahsante sana mke wangu!”
Wakakumbatiana kwa furaha. Tayari upande wa Laura hapakuwa na pingamizi. Ilibaki upande wa Chris tu.
***
Chris aliingia Dar es Salaam akiwa na matumaini mapya. Hakuwa na shaka yoyote kuhusu kumpata Laura. Alipozungumza na baba yake, alimwambia amwachie kila kitu yeye, anachotaka ni kuona anaoa!
“Zungumza na baba yako mdogo akamilishe kila kitu kuhusu ndoa. Kama mtaamua mnaweza kufunga ndoa ya kimila kijijini halafu kanisani mje mfunge huku Dar. Kutokana na majukumu yangu, namwachia jukumu hilo baba yako mdogo.
“Tafadhali lifanyike haraka sana. Mimi nimeshazungumza na marafiki zangu kuhusu ndoa yako. Wapo tayari kunisaidia. Wewe niachie mimi kila kitu, sawa?” akasema mzee Shila kwa kujiamini.
“Sawa baba, nimekuelewa!” akajibu Chris akiachia tabasamu.
Wasiwasi wa nini?
***
Siku zilikwenda haraka sana, hawakuwa na kitu cha kusubiri. Kwa kuwa Shamakala alikuwa anajua kila kitu kinachoendelea, kilichofanyika ilikuwa ni kupeleka posa kwa mzee Ngeleja.
Walilazimika kusafiri kutokea Singida mpaka Mwanza na kukamilisha zoezi la posa. Kila kitu kilikwenda sawa kabisa, posa ilikubaliwa na mahari ikapagwa. Vitu vidogovidogo vya kimila vilikamilishwa na mzee Ngeleja akawa tayari binti yake aende kufunga ndoa ya kimila kijijini.
Zoezi hilo lilifanyika bila wazazi wa pande zote mbili. Ndoa ilisimamiwa na Shamakala, baba mdogo wa Chris na wawakilishi wa mzee Ngeleja kutoka Mwanza. Baada ya hapo Laura alirudi chuoni kumalizia mitihani yake ya mwisho.
Mzee Shila alijulishwa na mdogo wake, Shamakala kuhusu mwenendo wa kila kitu kilivyokuwa kijijini. Alifurahi sana lakini kichwani mwake alijua kuwa, kijana wake alioa mwanamke wa nyumbani kwao jambo ambalo halikuwa la kweli.
***
Mipango yote ilivyokamilika, zoezi la mahari liliachwa mikononi mwa Shamakala. Yeye na washenga wa Chris ndiyo waliosafiri tena hadi Mwanza kulipa mahari kisha ikafanyika hafla fupi ya Laura kuvalishwa pete ya uchumba.
Kutokea hapo, Laura akawa mchumba rasmi wa Chris. Hadi kufikia muda huo, baba na mama wa Chris walikuwa hawajamuona Laura zaidi ya picha tu.
Mzee Shila hakutaka kusumbua watu, alikuwa ameshatayarisha fedha za kutosha kwa ajili ya sherehe ya mwanaye. Aliitisha kikao cha watu wachache tu, marafiki zake wa karibu kwa ajili ya kupeana mawazo ya namna harusi ya mwanaye itakavyokuwa na michango waliyoahidi.
Huko Mwanza vikao vya sherehe ya kumuaga Laura viliendelea. Taarifa ambazo mzee Shila alizipata ni kwamba, sherehe ya kumuaga Laura ingefanyika jijini Mwanza kwa baba yake mdogo ambapo aliishi na kusoma huko kwa muda mrefu.
Hata hivyo, baadaye siri ilivuja! Mzee Shila akagundua kuwa Laura hakuwa Mnyiramba, wala hakuwahi kuishi Mpambala kama ilivyoelezwa lakini pia hakuitwa Njile.
Ni Msukuma wa Mwanza!
Mzee Ngeleja alikasirika sana. Ilibaki wiki chache sana kabla ya ndoa. Alimwita Chris nyumbani kwake ambaye alimkuta baba yake amewaka kwa hasira.
“Chris unawezaje kunifanyia maigizo?” akafoka kwa hasira mbele ya mwanaye Chris.
“Kivipi baba?” Chris aliuliza lakini alianza kuhisi kuwa tayari mambo yalishaharibika.
“Huyo mchumba wako ni mtu wa wapi?”
“Baba jamani... si ni Singida!”
“Mpuuzi wewe! Singida ndiyo Mwanza siku hizi siyo? Halafu unanidanganya mimi kama mtoto mdogo? Pumbavu kabisa, sasa hiyo ndoa hesabu haipo.
Potelea mbali fedha nilizopoteza, lakini safari hii nitaongozana na wewe hadi kijijini na nitahakikisha unaoa mwanamke kutoka kijijini!” akasema mzee Shila kwa hasira.
ITAENDELEA
No comments