Simulizi : Singidani Sehemu Ya kumi na moja (11)
Akaamua kulala bila kuzungumza na mpenzi wake; si juu ya tukio lililotokea muda mfupi uliopita, bali hakutaka kuzungumza naye kitu chochote.
Akiwa anajitahidi kuubembeleza usingizi, simu yake iliita. Haraka akatupa macho yake kwenye kioo cha simu yake, akakutana na jina la ‘My Love’.
Alikuwa ni Chris. Alisita kupokea. Alishindwa kuelewa kama angepokea angezunguza nini na mpenzi wake. Habari alizokuwa nazo, hazikuwa nzuri hata kidogo. Ni habari ambazo asingependa kuzisikia kabisa.
“Lakini sijui anataka kuniambia nini...acha tu nimpokelee,” mwisho akapitisha uamuzi huo.
Akapokea.
“Hello darling,” ilikuwa sauti ya Chris.
“Niambie mpenzi wangu,” Laura alijitahidi kuzungumza kwa upendo akiweka pembeni tatizo lilitokea.
“Nimeshindwa kulala kabisa bila kuzungumza na wewe. Nimeshtuka muda huu mpenzi, nikakukumbuka,” akasema Chris.
“Kweli mpenzi wangu?”
“Kabisa dear.”
“Nashukuru kusikia hivyo, wazee hawajambo?”
“No! Kwa muda niliofika, ilikuwa vigumu sana kwenda nyumbani. Nipo kwangu Kijitonyama. Vipi huko, wewe?”
“Hawajambo.”
“Umewagusia suala letu?”
“Hapana mpenzi, nimeona nilale kwanza, niwaambie kesho. Ulipenda iwe leo mpenzi wangu?”
“Kabisa.”
“Mh! Una haraka? Unatamani hata hiyo ndoa yenyewe ingekuwa kesho. Mimi ni wako tu mpenzi, wala usiwe na wasiwasi wowote. Mimi ni mali yako.”
“Kweli?”
“Kwa nini usiamini maneno yangu?”
“Nakuamini mpenzi.”
“Nashukuru kusikia hivyo, nakutakia usiku mwema, nitakutafuta kesho mpenzi wangu sawa.”
“Sawa baba.”
“Usiache kunijulisha chochote kitakachotokea kuhusu mambo yetu.”
“Sawa mpenzi wangu.”
Wakakata simu zao.
Kitendo cha kukata tu simu, ilikuwa kama ndiyo tiketi ya Laura kuanza kulia. Alilia kuliko kawaida. Aliumizwa sana na maneno ya Chris ambaye hakujua kilichokuwa kikiendelea Mwanza!
Ukweli ni kwamba, Chris hakutakiwa kwa sababu tu alikuwa msanii wa filamu.
Kwa mama yake na Laura, msanii wa filamu ni mhuni tu, asiye na sifa ya kummiliki mwanaye.
Ulikuwa mwiba mkali sana kwa Laura ambaye aliugulia mwenyewe. Hakuwa na wa kumwambia kuhusu kilichokuwa kikiendelea.
Alilia sana.
Mto wote ulikuwa chapachapa! Ulilowanishwa na machozi ya Laura. Alikuwa na jeraha kubwa sana moyoni mwake. Jeraha bichi kabisa. Jeraha linalovuja damu!
***
“Niambie ulipofikia,” mzee Shila, baba yake na Chris alimwambia mwanaye jioni hiyo walipokuwa wamepumzika bustanini.
Siku nzima Chris aliamua kushinda nyumbani kwao, Mbezi Beach. Hakwenda kazini wala hakukutana na rafiki zake. Aliamua kujipumzisha na ndugu zake nyumbani.
“Hatua nzuri baba. Bibi ameshamaliza kila kitu. Imebaki ndoa tu,” akasema Chris.
“Kweli?”
MOYONI Chris alikuwa na woga ambao hauna kipimo, alijua wazi jibu ambalo angemjibu baba yake, lilikuwa la uongo lakini alilazimika kufanya hivyo kwa sababu ya kutimiza lengo lake.
Ni kweli alikuwa akidanganya lakini hata baba yake hakumtendea haki kumchagulia mahali na mtu wa kumuoa. Jambo hilo liligoma kabisa kuingia ubongoni mwake.
“Niamini baba, nasema kweli kabisa.”
Chris aliyatuliza macho yake usoni mwa baba yake, aliona milima midogomidogo iliyokuwa usoni mwa Mzee Shila ikiwa kama inaporomoka! Makunyanzi yake yakayeyuka taratibu.
Tabasamu likachanua!
Alitamani sana kuona mwanaye akioa! Siyo kuoa tu; aoe msichana kutoka kijijini! Kilichoendelea Mwanza, hakuna aliyejua!
Si Chris wala baba yake, mzee Shila.
Ni fumbo!
“Ahsante sana mwanangu. Naamini hujaniangusha, namwamini sana baba yako mdogo, najua hawezi kufanya makosa. Vipi, umeweza kuja na picha yake?”
“Hapana baba, ungependa kumuona?” akauliza Chris akitabasamu.
“Kabisa...natamani kumuona.”
“Nitafanya mpango wa picha, ngoja nifanye mawasiliano nitakujulisha.”
“Sawa mwanangu.”
Furaha ya mzee Shila ilikuwa wazi kabisa, ugomvi wa kwanza na mwanaye ulikuwa umeisha, ulibaki mmoja tu; kuigiza! Kwa mzee Shila, kuigiza ilikuwa ni uhuni na kujidhalilisha.
Kila alipokutana na skendo za wasanii mbalimbali katika magazeti, alijua kwa sababu mwanaye pia ni msanii, lazima angekuwa na tabia kama hizo. Siku zote alipata tabu sana kumfanya Chris akubaliane naye.
Hata hivyo, kwa hatua hiyo ya awali, kwa mzee Shila yalikuwa mafanikio makubwa. Moyoni akasema: “Acha kwanza hili lipite, mengine yataendelea. Hanishindi, huyu ni nimemzaa mwenyewe.”
Ilikuwa furaha kubwa sana kwa familia hiyo, siku nzima walishinda wakiwa wenye amani, kitu kikubwa kilichojadiliwa, ilikuwa ndoa ya Chris na Njile (Laura).
“Sikupatii picha mwanangu...siku hiyo, nakuona umevaa suti yako safi na mkeo amependeza, ukumbi mzima unasubiri kusikia utambulisho wa wazazi wako. MC sasa anasema: Baba mzaa chema, Profesa Shila naomba usimame watu wakuone....” alisema mzee Shila akicheka.
“Hatimaye Dk. Chris ameoa, ah! Mwanangu kwa kweli itakuwa furaha kubwa sana kwetu,” akadakia mama yake.
Hakutaka kabisa vurugu siku hiyo, vikao vyake vya pombe na rafiki zake akina Jaybee, Ramsey na Chika, alivisamehe kwa siku hiyo.
***
Usiku mzima, Laura hakupata usingizi. Mawazo yake yalikuwa kwa Chris ambaye sasa ndoto za kuoana zilikuwa zimeanza kuyeyuka. Tegemeo pekee wa kumsaidia katika hilo alikuwa ni mama yake ambaye hakutaka kuwa upande wake kabisa.
Asubuhi aliamka mapema na kukaa sebuleni akijifanya anaangalia taarifa ya habari ya Runinga ya ITV. Baba yake, mzee Moses Ngeleja alitoka akiwa ameshajiandaa kwenda kazini.
Alipomuona mwanaye sebuleni, alitabasamu...
“Morning dad!” Laura akasalimia kwa Kimombo.
“Morning to you daughter. Vipi za masomo?”
“Nzuri tu baba, nimebakiza kipindi kifupi cha mwisho nimalize masomo kabisa.”
“Ni kweli. Naona Singida si kubaya, kumekupenda sana mwanangu.”
“Mh! Baba bwana...”
“Laura, acha mimi nikimbie kazini, jioni nitawahi kurudi kwa ajili yako. Nina mengi ya kuzungumza na wewe mwanangu.”
Hayo yalimfanya Laura aamini kuwa mpaka muda huo, mama yake alikuwa hajamwambia chochote baba yake.
“Ila dad, natamani uniruhusu nije nikuone ofisini kwako mchana, naona jioni ni mbali, nami nina yangu ya kuzungumza na wewe.”
“Sawa...karibu mwanangu!”
Mzee Ngeleja akatoka nje. Akaingia kwenye gari yake aina ya Toyota VX, akaelekea kazini kwake, katikati ya Jiji la Mwanza, Jengo la Kaijage ilipokuwa ofisi yake.
***
Laura hakutaka kuzungumza na mama yake chochote kuhusiana na suala la Chris. Hata mchana alipotoka kwenda ofisini kwa baba yake, hakumwambia ukweli, zaidi ya kumdanganya kuwa anakwenda kumuona rafiki yake.
Akiwa mbele ya meza ya baba yake, Laura alijikaza na kumweleza baba yake ukweli: “Baba nimekua sasa, nimempata mkweo. Kuna mwanaume anataka kunioa.”
Mzee Ngeleja akatabasamu!
“Habari njema kiasi gani binti yangu. Vipi, umeshazungumza na mama yako kuhusu hili?” akasema mzee Ngeleja akiachia tabasamu mwanana usoni mwake.
USO wa Laura ulisawagika. Alionekana dhahiri kuwa na hofu ya ghafla. Mabadiliko yake yalikuwa wazi. Mzee Ngeleja alijua kwa vyovyote vile, kuna jambo lilimsumbua mwanaye.
“Laura...” Mzee Ngeleja akaita.
“Abee baba.”
“Vipi, mbona kama umebadilika kidogo?”
“Hapana.”
“Mh!” mzee Ngeleja akaguna.
“Mbona unaguna baba?”
“Mimi nakujua vizuri mwanangu, kuna kitu unanificha.”
“Hakika hakuna kitu baba.”
“Sawa, hebu turudi katika suala lako. Umeshazungumza na mama yako?” akamwuliza tena.
“Yaani baba hiyo ndiyo sababu iliyonifanya nije kuzungumza na wewe huku kazini kwako.”
“Kivipi?”
“Jana usiku nilijaribu kumweleza juu ya jambo hilo lakini cha ajabu, akapingana na mimi. Amesema hataki kusikia hizo habari.”
“Hawezi kusema hivyo ikiwa hana sababu. Hebu kuwa wazi, niambie tatizo ni nini?”
“Ukweli baba tatizo ni juu ya mwanaume mwenyewe. Unajua baba, huyo jamaa anayetaka kunioa ni msanii wa filamu, lakini siyo mhuni kama mama anavyofikiri.
“Ni msomi, tena daktari na anafanya kazi hospitalini kabisa ila anafanya filamu kama sehemu yake ya kujifurahisha tu.”
“Ni nani?”
“Jina lake halisi ni Christopher Joseph Shila, kwenye kazi zake za filamu anajiita Dk. Chris. Tumechunguzana kwa muda mrefu sana, namjua vizuri baba. Nimewahi kufika hadi kijijini kwao.
“Ni mwanaume sahihi kabisa baba, lakini mama ananikataza kwa vile tu ni msanii wa filamu, ndiyo maana nimeamua kuja kukushirikisha hili suala ili unisaidie,” alisema Laura mfululizo, baba yake akiwa kimya akimsikiliza.
“Ok! Nimekuelewa vizuri sana. Umesema nyumbani kwao ulikwenda. Ilikuwaje?”
“Hiyo ni habari nyingine baba, unajua kwao, wazazi wake nao walimpa masharti kuhusu mwanamke wa kuoa. Wakamwambia ni lazima mkewe atokee kijijini tena vijiji vya nyumbani kwao. Lakini kwa sababu sisi tunapendana ikabidi atumie mbinu nyingine ili kuwafanya wazazi wake waamini kuwa mimi ni wa kijijini.”
“Mkafanyaje sasa?”
Laura akamsimulia kila kitu kilivyokuwa bila kumficha chochote. Mzee Ngeleja alikuwa kimya akimsiliza mwanaye ambaye hakuna alichodanganya. Alionekana kumuelewa binti yake.
“Kwa hiyo huyo kijana anaishi Dar?”
“Ndiyo.”
“Na wazazi wake?”
“Dar pia.”
“Anaishi nao?”
“Hapana. Chris yeye amepanga kwake.”
“Hoja za mama yako zinaweza kuwa na maana lakini na wewe pia maelezo yako ni ya msingi. Sitaki kuwa dikteta katika hili. Kitu pekee ambacho nakitaka, ni kukutana na huyo kijana kwanza. Anaweza kuja hapa Mwanza nikaonana naye?” akasema mzee Ngeleja.
Laura akashtuka sana!
INAENDELEA
No comments