Simulizi : Singidani Sehemu YaKumi (10)
ILIONEKANA kama ni siku mpya kwao. Ilikuwa kama ndiyo kwanza wamekutana kwa mara ya kwanza katika mazingira waliyokuwa asubuhi hiyo.
Kila mmoja alijitahidi kumfanya mwenzake aone hakukosea kuwa naye katika muunganiko huo. Walionyeshana kazi!
Asubuhi hiyo upepo ulipuliza kwa kasi na kukifanya chumba kiwe baridi kabisa kama vile waliwasha kiyoyozi!
Hawakuhitaji blangeti! Wenyewe walitosha kwa kila kitu. Wote wakamiminiana misifa, ahadi kibao zikawatoka vinywani mwao.
Waliwaza ndoa tu!
Walishinda siku nzima ndani ya chumba hicho. Jioni, Chris alilazimika kuondoka na kurudi Mkalama. Mazungumzo ya usiku huo yaliendelea kuwa yaleyale. Laura alitawala.
“Mjukuu wangu, usiache kumuoa huyo msichana. Ni mzuri na anakufaa kwa maisha yako,” alisema bibi.
“Usijali bibi, hilo nakuahidi. Halafu kesho ndiyo narudi Dar. Najua unataka kusema kitu... bibi kazi nyingi lazima niondoke ila nitakuacha vizuri,” akasema Chris akitoa bahasha ya khaki na kumkabidhi.
“Ni laki moja bibi, tena nimezichenji kabisa. Zipo noti za elfu mbilimbili, najua hizi zitakusaidia mpaka siku nitakapokuja tena huku kijijini.”
Bibi aliachia mdomo wazi kwa furaha. Alisimama kwa tabu na kumkumbatia mjukuu wake.
“Mungu akubariki mume wangu, kwenye riziki zako kuongezeke,” akasema bibi.
“Ahsante sana bibi, nashukuru sana.”
Chris aliachana na bibi, akatenga muda wa kutosha kuzungumza na baba yake mdogo, Shamakala. Kama ilivyokuwa kwa bibi, ndivyo alivyofanya kwa Shamakala.
Alimpatia kiasi cha shilingi laki moja kama ahsante ya mambo yote aliyomsaidia.
“Kuondoka?” akauliza Shamakala.
“Kesho.”
“Sasa mwenzako?”
“Nimeshampa maelekezo, nimemwambia mhudumu wa pale amwamshe usiku saa tisa, hata mimi nitampigia. Huyo atamsaidia kumpakia kwenye gari ambapo atanikuta kituoni Mkalama.”
“Wazo zuri.”
Uzuri ni kwamba, gesti aliyokuwa amefikia Laura ilikuwa barabarani kabisa. Ilikuwa ni kiasi cha kuamshwa na kuwa barabarani mapema.
Kwa kawaida, magari ya kwenda mjini hutoka kituo cha Ibaga, usiku wa saa tisa na nusu. Kila siku kulikuwa na gari moja tu, likikukuacha, inabidi usibiri mpaka kesho yake au ukodi pikipiki, gharama yake wengi huikimbia.
Usafiri wa kutokea Ibaga, huwa ni kwenda Singida Mjini, Arusha kupitia Hydom, Igunga na Meatu kwa magari tofauti. Jambo hilo Laura alijulishwa mapema na mpenzi wake, kwa hiyo alijiandaa!
***
Chris alidamka mapema sana. Saa nane na nusu, tayari alikuwa macho. Haraka akampigia Laura ambaye alipokea na kumjulisha kuwa ameshaamka muda mrefu uliopita.
Alijiandaa haraka kisha akatoka na kwenda kumgongea baba yake mdogo, ambaye alitoka nje haraka. Tayari ilikuwa nimeshafika saa tisa kamili usiku.
Kwa msaada wa tochi, waliweza kutembea taratibu kuelekea barabarani. Walitumia robo saa kufika eneo hilo. Ilipotimia saa kumi kasorobo usiku, mlio wa gari ulianza kusikika kwa mbali, walikuwa na uhakika kuwa basi la kwenda mjini lilikuwa linakaribia kufika.
“Gari hilo linakuja,” akasema Chris.
“Ni kweli, ndiyo mida yake hii. Mimi nakutakia kila la kheri, hakikisha unatimiza yote tuliyokubaliana.”
“Sawa baba mdogo, nakutegemea.”
Basi lilisimama mbele yao, Chris akaingia. Hakupata shida kujua alipokuwa amekaa mpenzi wake, maana tayari alikuwa ameshakata tiketi mapema.
“Pole na usingizi mpenzi,” akasema Chris.
Laura akatabasamu, akamjibu: “Ahsante.”
Ni kama alikuwa anasubiri shuka katikati ya usiku wenye baridi kali. Alijitupa kifuani mwa Chris, akatulia. Robo saa baadaye, alikuwa ameshapitiwa na usingizi.
Alishtuka walipofika Iguguno! Tayari kulikuwa kumekucha! Muda mfupi baadaye walishuka Singida Mjini. Hapo ndipo walipoachana kwa majonzi mazito.
Chris alipanda basi lililotoka Kahama kwenda Dar na Laura akapanda basi lililotoka Dodoma kwenda Mwanza. Walishindwa kuficha hisia zao, muda mfupi kabla hawajaachana, walikumbatiana kwa muda mrefu. Kila mmoja alimhitaji mwenzake.
Mapenzi matamu kiasi gani?
WA kwanza kuingia kwenye basi alikuwa Chris aliyeingia kwenye Basi la NBS. Chris alitoa kichwa dirishani, akampungia mkono Laura, naye akafanya hivyo. Chris alisisimka alipoona mashavu ya mpenzi wake yakitiririsha machozi!
Hakuweza kuvumilia zaidi, akarudisha kichwa chake ndani kisha haraka akachukua simu yake na kumwandikia ujumbe uliosomeka: “Usilie mama, unanifanya nijisikie vibaya. Najua unanipenda sana Laura, nakupenda pia!”
“Najua Chris, lakini maumivu. Nimekuzoea sana, kwa siku chache nilizokaa nawe kijijini zimekuwa za tofauti sana kwangu, nahisi kama tayari umeshanioa. Nakupenda sana.”
“Nakupenda pia.”
Waliendelea kuwasiliana kwa muda mrefu. Tayari Laura alishangia kwenye Basi la Mohammed lililotokea Dodoma kuelekea Mwanza.
Safari nzima kwao ilikuwa yenye furaha kubwa. Ni kama walikuwa wakisafiri umbali mfupi tu kutokana na kuwekana karibu kwa mawasiliano.
Ahadi yao ilikuwa moja tu; ndoa. Wote waliazimia kuungana katika ndoa takatifu.
***
Chris aliingia Dar es Salaam saa mbili usiku akiwa amechoka sana. Alichokifanya ni kuchukua teksi iliyompeleka nyumbani kwake Kijitonyama.
Kweli alikuwa na hamu sana ya kukutana na wasanii wenzake akina Jaybee, Ramsey na Chika lakini kwa uchovu aliokuwa nao ilikuwa lazima apumzike kwanza.
Alijimwagia maji, akatafuta chakula kwenye mgahawa wa jirani, kisha akarudi nyumbani alipofungua jokofu lake na kutoa kinywaji. Ilikuwa lazima ajitoe uchovu kidogo!
Bia tatu zilitosha kumwondolea uchovu aliokuwa nao awali. Akajilaza kitandani akiendelea kutafakari siku yake mpya itakayofuata!
***
Mapokezi ya Laura nyumbani kwao Nyakato, Mwanza yalikuwa mazuri sana. Usiku mzima alikuwa akizungumza na ndugu zake ambao hakuonana nao kwa muda mrefu alipokuwa masomoni.
Sebule yao ilichangamka sana. Mpaka usiku sana, wengi walikuwa wameshaingia vyumbani kulala, wakabaki Laura na mama yake tu.
Hapo ndipo Laura alipoamua kutumia nafasi hiyo vizuri kwa ajili ya kuzungumza na mama yake. Walikuwa wawili tu.
“Mama kuna kitu nataka kukuambia!” akasema Laura akimwangalia mama yake usoni.
“Niambie mwanangu, ni nini tena hicho?”
“Nimepata mchumba... anataka kunioa.”
“Unasema?”
“Nimepata mchumba mama.”
“Ni nani?”
“Yupo Dar.”
“Umekutana naye wapi?”
“Singida.”
“Naye ni mwanafunzi?”
“Hapana mama. Nipe nafasi nikueleze vizuri, tatizo una haraka sana. Kwa nini hutaki kunisikiliza kwanza? Halafu tatizo si huyo mvulana, kuna shida kidogo kwa upande wa wazazi wake.”
“Shida kivipi?”
“Wazazi wake wamemwambia lazima aoe kijijini lakini sisi tumependana na yupo tayari kunioa.”
“Hata kama mmependana na yupo tayari kukuoa, itawezekana vipi wakati wazazi wake hawataki?”
“Kuna mpango tumeshafanya. Hivi ninavyoongea na wewe, tayari nimeshafika hadi kijijini kwao na wamenikubali.”
“Mh!”
“Usigune mama, ngoja nikueleze vizuri.”
Laura alimsimulia mchezo mzima ulivyokuwa, jinsi jambo hilo alivyoshirishwa baba yake mdogo na Chris, Shamakala, bila bibi na ndugu zake wengine kufahamu.
“Mh! Una hatari wewe mtoto. Enhee, huyo kijana mwenyewe ni nani hasa? Na kweli umri wake unamruhusu kuoa?” akauliza mama Laura.
“Hana shida, ni mtu mzima. Ana miaka 35 sasa, nayaamini maamuzi yake mama.”
“Anaitwa nani?”
“Ni Dk. Chris yule msanii wa filamu, kwa sababu ni maarufu najua utakuwa unamfahamu,” akasema Laura akitabasamu.
Alitegemea mama yake angefurahia jambo hilo, alichokutana nacho kilikuwa tofauti kabisa:
“Unasemaje wewe?” mama Laura akasema kwa sauti ya ukali sana.
“Vipi tena mama?”
“Sitaki matatizo na baba yako, unataka kuolewa na hao wahuni wa filamu? Huo ujinga wako uishie hapahapa,” alisema mama Laura kwa hasira kisha akaondoka sebuleni na kumuacha Laura peke yake!
Huzuni mpya!
ALIHISI moyo wake kama umeingiwa na ubaridi mkali, Laura alichanganyikiwa kwa hakika. Kwa urafiki wake na mama yake, alijua jambo lile angelipokea kwa urahisi sana.
Kinyume na matarajio hayo, mama yake aligeuka mbogo! Maneno yake yakamchanganya sana. Wasanii ni wahuni? Aliumia sana kichwani mwake.
“Wasanii ni wahuni? Mbona simwelewi mama lakini? Labda ni kweli ni wahuni lakini si kwa Chris wangu. Chris si mhuni. Kwanza ni daktari. Mama lazima akubaliane na mimi.
“Siwezi kukubali kuishi na mtu mwingine tofauti na Chris. Sijamwelewa mama hata kidogo. Hapo nitapingana naye,” aliwaza Laura.
Furaha aliyokuwa nayo moyoni mwake iliyeyuka ghafla. Alimtegemea mama yake ndiye angemuunga mkono na ugomvi na baba yake usingekuwepo lakini imekuwa tofauti.
Aliinuka kwa hasira na kwenda zake chumbani kwake. Hakufanya chochote zaidi ya kujitupa kitandani na kulala kama alivyotoka sebuleni.
Kitu pekee alichokumbuka ilikuwa ni kuchukua simu yake. Akaiweka karibu yake, pembeni ya mto. Alitakiwa kupunguza mawazo yake, mtu pekee ambaye angemsaidia kupunguza mawazo yaliyokuwa yamemvaa kwa kasi muda ule alikuwa ni mpenzi wake tu – Chris.
Lakini vipi kama angemwambia Chris kuhusu mama yake kugoma?
“Itakuwa tatizo lingine, sitakiwi kumwambia chochote,” akawaza.
“Pia sitakiwi kumpigia,” akawaza tena.
Sauti ya Chris pengine ingeweza kuwa dawa ya usingizi na kumpunguzia maumivu makali ya moyo lakini kwa namna hali ilivyokuwa, aliona ni bora aache kumpigia.
Alipitisha azimio hilo.
INAENDELEA
No comments