Simulizi : Singidani Sehemu YaTisa (9)

“Ni wazo zuri, utaongozana naye sasa au?”

“Ndiyo... mimi ndiyo mwenyeji wake pale, lazima niende naye.”

“Mimi naunga mkono mwanangu, sina matatizo na hilo.”
Simulizi ya singidani

“Sawa mama, nilisema nikujulishe tu maana ungeshangaa kuona mtu amekuja nyumbani bila taarifa yako, tukaona si busara.”

“Mmefanya vizuri.”

Shamakala alifurahishwa sana na majibu ya mama yake. Alimfuata Chris na kumweleza kila kitu kilivyokuwa, akafurahi sana.

Usiku ulikuwa mrefu sana, alitamani asubuhi ifike haraka ili Laura afike nyumbani kwao. Alitaka kuona namna ambavyo bibi yake angemchukulia.

***

Chris alikuwa wa kwanza kuamka asubuhi hiyo. Alidamka saa moja kasoro, muda ambao kwa kipindi hicho ambacho hakikuwa cha kilimo, ilikuwa mapema sana.

Kwa kawaida wakati wa kilimo wanakijiji hadaamka mapema na kwenda mashambani. Si katika kipindi hicho cha kiangazi. Alifanya shughuli ndogondogo za nyumbani hadi saa mbili ndipo baba yake mdogo alipoamka.

Chris alifurahi sana alipomuona baba yake mdogo akitoka nje. Baada ya salamu, wakaanza kupanga namna ya kufanya.

“Hapa hakuna cha kujadili sana, twende tu juu kule juu tukachukue pikipiki tuondoke,” akasema Chris.

“Sawa... lakini tupate kifungua kinywa kwanza.”

“Hapana, tutakunywa supu Ibaga.”

“Sawa.”

Hawakuwa na muda wa kupoteza, walikwenda barabarani walipochukua pikipiki moja ambayo walipanda kwa mtindo wa mshikaki, safari ya kwenda Ibaga ikaanza.

Kwa pikipiki ulikuwa ni mwendo wa dakika kumi tu, walikuwa wameshafika Ibaga. Chris ndiye aliyemlipa dereva, kisha wakatembea na kuelekea kwenye mgahawa mmoja maarufu eneo hilo.

“Sasa dingi, we’ nisubiri hapa, ngoja nikamchukue.”

“hivi ni wapi kwani?”

“Tumefikia Sayuni Lodge.”

“Sawa.”

Shamakala na Chris walikuwa na umri unaokaribiana sana, Shamakala alikuwa mtoto wa mwisho katika uzao wa baba yake na Chris. Sababu hiyo iliwafanya wazoeane kwa kiasi kikubwa.

Hata mazungumzo yao yalikuwa ya ujana zaidi kutokana na umri wao kukaribiana. Hata hivyo, hilo halikuvunja heshima waliyokuwa nayo. Bado Chris aliendelea kumheshimu Shamakala kama baba yake.

Chris alifika Sayuni na kwenda kugonga katika chumba alichomuacha Laura jana yake. Aligonga mara moja tu, Laura alifungua. Chris alishangaa sana.

Alikutana na Laura mpya kabisa. Laura alikuwa amevaa mavazi ambayo kwa kumwangalia tu unajua kuwa, alikuwa msichana aliyeishi kijijini. Alifafana nao kwa kila kitu.

“Daah! Kweli umefunika mpenzi wangu. Hapo umepatia kabisa.”
“Nashukuru mpenzi, nini kinaendelea?”

“Kama uko tayari, tuondoke. Hakuna kitu cha kusubiri zaidi.”

Ndivyo ilivyokuwa, walitoka na kwenda mgahawani alipokuwa Shamakala. Utambulisho mfupi ukafanyika kisha wote wakaagiza supu ya mbuzi. Walitumia dakika kumi tu kumaliza kula, kisha wote kwa pamoja wakainuka na kwenda kukodisha pikipiki iliyowafikisha kijijini Mkalama.

Safari hii walifikishwa hadi nyumbani kwao kabisa. Walishuka kwenye pikipiki kisha wakapiga hatua za taratibu huku nyuso zao zikiwa zimepambwa na tabasamu pana. Bahati nzuri bibi alikuwa nje ameketi kibarazani.

Bibi alipowaona, alionekana kuukunja uso wake. Hata Chris alipojaribu kutabasamu, bado bibi aliendelea kukunja uso wake.

HAKUaliyejua kilichokuwa moyoni mwa bibi, hakuwa ameukunja uso wake kwa hasira. Uso ulikunjamana kwa mshangao wa kumuona mjukuu wake sasa alifikia uamuzi sahihi wa kuachana na ukapera.

Chris na baba yake mdogo walipiga hatua za taratibu kumfuata bibi. Shamakala alikaa pembeni, bibi akawasogelea, wakakutana katikati. Alichokifanya bibi ilikuwa ni kuinama kidogo.

Haraka Shamakala akamwonyesha Laura ishara kuwa apige magoti chini. Akafanya hivyo. Bibi akamshika mkono Chris. Akatema mate kidogo mkononi mwake kisha akampaka Chris usoni.

Akamsogelea Laura, akamshika mikono yote miwili na kumwonyesha ishara asimame. Akafanya hivyo; akamvutia kwake na kumkumbatia, kisha akamtemea mate kidogo kwenye paji lake la uso.

Laura akatabasamu!


Kwao ilikuwa heshima kubwa sana, kutemewa mate na bibi, ilimaanisha baraka na kukubalika katika familia. Bibi akamshika mkono na kumwongoza hadi sebuleni, kwenye nyumba ile ya zamani ya tembe.

“Karibu sana mjukuu wangu,” bibi akamkaribisha Laura.

“Ahsante bibi.”

Tayari kifungua kinywa kilikuwa kimeshaandaliwa na mke wa Shamakala. Chai ilitengwa na vitafunwa vya maboga na mahindi ya kuchemsha. Wakaketi kwenye jamvi na kuanza kula. Wanaume walikula nje, wanawake ndani.



Ilikuwa siku mpya kwa Chris. Siku ya utambulisho wa ‘Laura wa Kijijini!’. Ukweli wa mambo ulijulikana na Laura, Chris na Shamakala pekee.



***

Moto ulikuwa unawaka huku moshi ukitoka. Ulikuwa usiku wa mbalamwezi. Watu wawili walikuwa wameuzunguka moto uliowashwa kwa kutumia kinyesi cha ngo’mbe. Ndani ya moto huo kulikuwa na karanga zikichomwa.



Kazi yao ilikuwa ni kuchomoa na kuendelea kula taratibu. Hapakuwa na mazungumzo. Muda kidogo bibi alifika.



“Hivi huyu msichana ni wa hapa Mkalama kweli?” bibi akamwuliza Chris.

“Hapana bibi. Ni kutoka Mpambala kama tulivyokuambia,” Chris akajibu.

“Lakini mbona hafahamu kinyumbani?”



“Bibi hajakulia hapa, wazazi wake walihamia Mwanza muda mrefu sana, tangu akiwa mdogo, amesomea huko na sasa hivi anamalizia masomo yake Singida Mjini ndiyo maana hajui vizuri kinyumbani. Ni kama mimi tu.”



“Hapo sawa.”

“Vipi lakini bibi, umegundua tatizo lolote kutoka kwake?”

“Tatizo? Hapana... ni msichana mzuri sana, mchapakazi na anayejua kujituma. Hana tatizo kabisa. Naweza kusema kwamba, mjukumuu wangu pale umepata mke sahihi.”



“Ahsante sana bibi.”

“Sasa lini mipango yako?”

“Bado kidogo, nasubiri amalizie masomo yake tu. Amebakiza miezi sita. Hatutakuwa na muda wa kusubiri zaidi. Akimaliza kinachofuata ni ndoa.”



“Sawa. Nyie endeleeni kuota moto lakini chakula kipo tayari, sasa hivi kinakuja.”

“Sawa bibi.”



***

Siku tatu zilitosha kabisa kwa Laura kuthibitishwa kuwa mke mtarajiwa wa Chris. Bibi alishatoa baraka zote. Ilikuwa furaha kubwa sana kwao. Waliagana wakiwa wenye furaha sana.



“Karibu kwenye ukoo wetu mjukuu wangu, hakuna atakayepinga uamuzi huu. Hata kama nikifika leo, kabla ya ndoa yenu, watu wote wanaonihusu watambue kuwa nimeridhia ndoa yenu,” akasema bibi.

“Ahsante sana bibi, nimefurahi sana kusikia hivyo,” Chris akasema.



Chris na Laura wakaondoka. Walikwenda hadi kituoni ambapo walichukua pikipiki iliyowapeleka moja kwa moja hadi mji mdogo wa Ibaga. Walifikia kwenye gesti ileile, Sayuni.



Walipoingia tu chumbani, wote walikumbatiana kwa furaha ya ushindi. Laura machozi yalimtoka kama maji yanavyotiririka kwenye mfereji uliopo bondeni.



“Tulia mpenzi, najua ni kiasi gani una furaha moyoni mwako. Ni furaha yetu sote na ni haki yetu kufurahi,” akasema Chris.



“Sikutegemea kama mambo yangeisha kwa wepesi kiasi hiki.”

“Najua lakini usijali. Sasa tumebakiza eneo moja tu. Nyumbani kwenu. Lazima hili jambo lijulikane mpenzi wangu kama kweli tuna lengo la kuoana. Kuna kitu lazima kifanyike mpenzi.”



“Ni kweli baba, nakuamini kwa mawazo yako, tunaanzia wapi?”

“Nashauri tukitoka hapa, wewe usikae kabisa mjini, nenda moja kwa moja Mwanza, kazungumze na wazazi wako kuhusu hili suala ili nao pia wawe wanajua.


Maadamu tunapendana na bibi amesharidhia, naamini ni jambo jepesi sana kumhadaa mzee Shila!”

“Kweli dear?”“Kabisa!”“Sawa.”


Ikawa asubuhi nyingine yenye kupendeza zaidi. Furaha yao haikubaki mioyoni mwao pekee, ilitoa msukumo mkali na kuchemsha damu za miili yao. Wote wakawaka!

Walijua namna ya kukitumia chumba kile vizuri kabisa!

ITAENDELEA

No comments

Powered by Blogger.