Simulizi : Singidani Sehemu Ya Pili (2)

Simulizi ya singidani
ILA kilichotokea ukumbini mle alihisi ni kama alikuwa ndotoni. Ukweli haukuwa huo, hakuwa anaota. Kila kitu kilikuwa yakinifu kwa hakika kabisa.

Akaufaidi uzuri wa yule msichana kwa karibu kabisa. Moyoni alikuwa na furaha akijua kuwa angalau alikuwa akielekea kutimiza lengo lake. Kukaa naye pale pekee kulimpa matumaini mapya.

“Samahani kaka Chris,” akasema yule msichana kwa sauti iliyojaa utulivu na unyenyekevu.

“Achana na samahani...unaitwa nani mrembo?”

“Naitwa Laura.”

“Nice name...sikia...sitaki kukupotezea muda wako. Kikubwa ni kwamba nahitaji kuzungumza na wewe. Si hapa club na ujue kabisa ni mambo ya kazi,” akasema Chris kwa uhakika kabisa.

Laura akatulia kwa muda.

Muda huu sasa, Laura alipata nafasi nzuri ya kumwangalia Chris kwa ukaribu. Aliyafumbua macho yake makubwa yaliyozungushwa na wanja hafifu mweusi na kuyatuliza usoni mwa Chris.

Kuna kitu kipya aligundua; Chris alikuwa mwanaume mwenye wivu na aibu kidogo. Ukimya na uso wake uliojaa bashasha ulizidi kumpa matumaini kuwa amekutana na mwanaume makini.

“Umesema kazi?” akauliza haraka kama aliyegutuliwa mawazoni.

“Ndiyo.”

“Mimi nasoma.”

“Najua lakini unaweza kufanya kazi nje ya masomo yako.”

“Mh! Kazi gani?”

“Sanaa.”

“Unamaanisha filamu?”

“Ndiyo! Wewe ni msanii mkali sana, hujapata nafasi tu. Unaweza kuwapindua wasanii wote wanaotamba Bongo Movies sasa hivi. Niamini mimi. Unaweza sana ni kiasi cha kupewa nafasi na kuelekezwa kidogo sana, utakuwa mkali.”

“Unataka tuzungumze lini?”

“Leo, maana kesho nasafiri kwenda Mkalama.”

“Mkalama ni wapi?”

“Yaani hujui wilaya ambayo ipo katika mkoa unaoishi?”

“Mimi ni mwanafunzi tu hapa, natokea Mwanza. Kule ndiyo kwetu. Niambie kuhusu Ilemela, Sengerema, Kwimba, Ukerewe, Magu, Nyamagana na Misungwi nitakuambia lakini hapa najua hapahapa mjini tu labda sana Ikungi na Manyoni.”

Chris akacheka.

“Haya mama, nimekuelewa vizuri sana. Namaanisha usiku huu.”

“Tukazungumzie wapi sasa?”

“Hotelini.”

Laura akafura!

Macho ya Laura ni kama yalijitokeza yote yalipojificha. Yalizidi kuwa makubwa na kuchambua kope zake zilizotingishika kwa kasi kutokana na kufumba macho na kufumbua mara kwa mara.

Sura ya Laura ilionekana wazi kabisa kuchukizwa na maneno aliyoyasikia kutoka kwa Chris. Alimwangalia kwa dharau kidogo, akimchambua kuanzia chini hadi juu.

“Chris kumbe uko hivyo?” akauliza Laura kwa hamaki.

“Nikoje?”

“Sikia nikuambie, mimi siyo malaya kama unavyonichukulia. Nimekuja club kwa pesa yangu na nitaondoka mwenyewe baadaye kwa muda wangu lakini huwezi kunipata kirahisi hivyo kwa sababu sijui ya pesa zako au kwa vile unajulikana. Mimi siyo wa hivyo. Umekosea njia!”

“Unanifikiria vibaya Laura. Mimi si mwanaume wa namna hiyo. Tafadhali usinipe sifa ambayo si yangu. Naomba unielewe, lengo langu ni kazi tu, hakuna kitu kingine.

“Inawezekana hujajua thamani ya kipaji ulichonacho au hakuna aliyewahi kukuambia kuwa kuna kitu kama hicho ndani yako. Lakini pia inawezekana umeathiriwa na tabia ya wanaume wengi, wakitaka kumsaidia mwanamke lazima wawe wapenzi kwanza...that’s not me!”

“Sasa kwa nini unataka iwe hotelini?” Laura akamwuliza akimkazia macho.

“Vizuri sana. Kwanza ni kwa sababu ndipo nilipofikia lakini pia kuna utulivu mkubwa zaidi ya hapa.”

“Lakini mbona hata hapa tunaweza kwenda kuzungumzia nje?”

“Laura tafadhali heshimu mawazo yangu na unatakiwa kujua kuwa utakuwa salama kwa kila kitu. Tafadhali naomba ukubali.”

“Sawa tutakwenda kuzungumza hotelini lakini kwa masharti!” akasema Laura sasa kwa utulivu.

“Paaaaaa!” moyo wa Chris ukapiga kwa nguvu.



SHINDI ulianza kunukia. Kukubaliwa tu na msichana yule kwenda naye hotelini kwa mazunguzo ilikuwa sehemu ya ushindi. Potelea mbali kuhusu masharti aliyosema angempa, yasingemshinda!

“Kwanza masharti yapi?” akajiuliza Chris.

“Hana cha kunishinda huyu,” akazidi kuwaza.

Tabasamu changa lilichanua usoni mwa Chris wakati akizidi kufaidi uzuri wa macho ya msichana yule wa kuvutia; Laura! Kama kungekuwa na mashindano ya kumsaka mwanamke mwenye mvuto hasa wa kike, Laura lazima angeshinda.

Nini hana?

Angalia miguu yake. Hebu mtazamo anavyozungumza kwa mpangilio mzuri. Ona nyusi zake, angalia kiuno. Mwone hata mikono yake laini, mizuri inayoshawishi.

Laura ni mwanamke wa haja. Hana upungufu wowote kwa kumwangalia. Chris alivuta pumzi ndefu sana, kisha akazishusha taratibu. Akanyanyua glasi yake yenye pombe kali na kuipeleka kinywani.

Ilikuwa kali lakini hakujali. Aliifuta yote, aliposhusha glasi chini, ilikuwa tupu! Laura akawa anaangalia sinema ya bure. Akaachia tabasamu changa la kupendeza.

“Sawa kaka Chris?” Laura akauliza.

“Bila shaka Lau.”

“Mbona hujauliza kuhusu masharti?”

“Sina shaka kabisa na masharti yako, najua nitayamudu tu.”

“Unajua ni nini?”

“Kwanza utanirudisha chuo...” akasema Laura kwa sauti ya kudeka.

“Hilo limepitishwa bila kupingwa....lingine?”

“Hatutafanya chochote.”

“Wewe! Chochote lazima tufanye, maana tunakwenda kuzungumza.”

“Mi’ sitaki!”

“Hutaki?”

“Ndiyo sitaki.”

“Sasa mbona umekubali kwenda hotelini?”

“Nimekubali kwa ajili ya mazungumzo tu.”

“Sasa kwani hayo mazungumzo siyo chochote?” akauliza Chris.

Sura ya Laura iliyokuwa imekunjamana sasa ikarudi kawaida kabisa. Tabasamu likaonekana. Uzuri wake ukazidi kuchanua.

“Tuondoke zetu basi!” akasema Chris.

“Poa, twende.”

Waliongozana hadi nje, wakashikana mikono kama vile walikuwa wakifahamiana kabla. Laura alijishangaa sana kumzoea Chris kwa muda mfupi kiasi hicho.

Macho ya watu wote yalikuwa kwao. Tatizo ni umaarufu wa Chris. Moja kwa moja hadi kwenye taksi. Wakaingia.

“Wapi brother?”

“Aqua Vitae Resort.”

“Buku tano tu.”

“Endesha gari kaka.”

Dereva ni kama alikuwa amechanganyikiwa. Haraka akawasha gari na kuliondoa kwa kasi kuelekea Aqua Resort.

***

Chumba kilikuwa kikubwa, kizuri chenye hewa safi iliyochanganyika na manukato hafifu yasiyokera pua. Chris alikuwa amekaa kitandani na Laura kwenye sofa kubwa! Taa chumbani mle ilikuwa ya rangi hivyo kumfanya Laura azidi kuonekana katika mwonekano wa kuvutia zaidi.

Kitanda kilikuwa kikubwa, chenye mito mikubwa minne iliyopangwa vizuri kitandani. Mashuka meupe nayo yalizidi kukifanya chumba kionekane nadhifu zaidi.

Ni saa nane za usiku!

“Karibu sana Laura,” akasema Chris.

“Ahsante sana.”

“Kikubwa nilichotaka kukuambia ni kwamba wewe ni mrembo sana na unaweza kufanya vizuri kwenye sanaa kama ukiwezeshwa na kupewa mwongozo mzuri. Nakuambia ukweli, kuna uwezekano mkubwa sana wa kumfunika hata Wema au Johari.

“Niamini mimi, uwezo wako ni mkubwa sana Laura. Kubali nikusaidie tafadhali. Isitoshe nina sinema yangu mpya ambayo naiandaa, kuna sehemu ndani yake inahitaji sana msichana kama wewe. Nakuhakikikishia wewe ni staa na maisha yako yanaweza kubadilika ukitumia kipaji chako ipasavyo,” akasema Chris kwa sauti ya taratibu sana.

Shoti ya umeme wa mapenzi ilimwingia moyoni. Ilikuwa nafasi kubwa na muhimu sana kwake. Hakutakiwa kufanya ajizi katika nafasi ile ya pekee. Msichana mrembo kama Laura kuingia chumbani kwake halafu aondoke hivihivi?

“Kaka Chris, kweli mimi naweza kuwa msanii? Naweza kuwazidi hata mastaa?”

“Kabisa...niamini mimi. Ni marekebisho madogomadogo tu.”

Chris aliwaza kwa muda, alitakiwa kuwa na mbinu za kisasa ili aweze kumpata Laura. Lakini alijihakikishia moyoni kwamba alimpenda kwa dhati ya moyo wake. Kumpata kwa usiku ule tu halikuwa jambo muhimu kwake, alimtaka kwa maisha yake yote!

“Lakini nikimkosa usiku huu, sitaeleweka. Anaweza kuniona sijakamilika,” akazidi kuwaza Chris.



CHRIS aliinuka kitandani lakini akiwa tayari ameshainuka, akajishangaa maana hakujua aliinuka ili kufanya nini! Hakutaka kuonekana kama alikuwa hajui cha kufanya.

Akamwangalia Laura kwa jicho lililojaa ubembe, kisha akamsogelea na kukaa kwenye sofa kubwa lililotosha kukaliwa na watu wawili tu, akapiga magoti chini yake.

Bado hakujua alichotaka kumwambia. Bahati nzuri, Chris alikuwa na utajiri wa maneno kwa hiyo haikumpa shida sana. Laura akashangazwa na namna Chris alivyopiga magoti mbele yake.

“Sikia nikuambie Laura. Mimi ni mwanaume wa tofauti sana. Mara zote nimekuwa mkweli na ninayeheshimu hisia zangu. Kila kinachotoka kinywani mwangu, huwa yakinifu kabisa,” akasema Chris, kisha akatulia kidogo.

Ni kama alikuwa akifikiria jambo. Kichwani Laura akaanza kuona hisia za mapenzi kutoka kwa Chris kwenda kwake. Pamoja na kwamba alikuwa ameonja kidogo kilevi, hakuwa tayari kumpa Chris mwili wake kwa sababu tu ni staa wa filamu.

Alifika pale hotelini kwa heshima tu. Alimwamini ghafla sana. Hakutegemea kama angetongozwa na hata kama angetongozwa, hakuwa tayari kujiachia kwa siku hiyohiyo!

“Ameanza....nilijua tu. Wanaume bwana!” akawaza Laura.

“Lakini hapati kitu hapa,” akawaza tena.

Chris akaendelea: “Shika haya maneno yangu Laura. Nayaona maisha yako miaka miwili ijayo, jinsi utakavyokuwa staa na maisha yako yatakavyobadilika.

“Acha nikutengeneze. Najua ninaweza kukufanya ukawa juu kuliko unavyowaza. Unacho kipaji kikubwa sana Laura.”

Chris alikuwa akizungumza kwa hisia kali sana. Hata hivyo si kweli kwamba, Laura alikuwa na kipaji cha kuigiza – alikuwa mrembo! Hiyo ilikuwa gia tu ya kumwingiza kwenye kumi na nane zake.

Laura aliachia tabasamu pana. Moyoni Chris akaugulia maumivu ya shoti ya mapenzi. Alizidi kuchanganyikiwa. Kila dakika, kila sekunde, uzuri wa Laura uliongezeka.

Pamoja na kuelezwa yote hayo, Laura hakuzungumza chochote. Alibaki kimya tu akimwangalia Chris. Macho yao kuna wakati yaligongana na wote hawakuweza kuhimili kuangaliana japo kwa sekunde tano tu mfululizo.

Tayari kuna kitu kilianza kuingia moyoni mwa Laura lakini hakukiamini sana. Eti ameanza kumpenda Chris!

“Siyo kweli. Hizi si hisia zangu. Ni pombe tu,” akawaza.

Ghafla Chris akasimama. Alifanya kitendo hicho kwa haraka sana kama aliyeamrishwa. Alirudi nyuma kidogo hadi alipofikia kitandani. Akachukua taulo kubwa pale kitandani kisha akalitupa begani mwake.

“Samahani...” akasema Chris.

“Ndiyo!”

“Naingia bafuni kidogo.”

“Sawa.”

Chris akapiga hatua nyingine fupi, akaufikia mlango wa kuingia bafuni. Akashika kitasa na kukinyonga kidogo. Mlango ukafunguka. Mara moja akaingia, halafu akaufunga.

Punde tu maji yalianza kusikika yakichuruzika. Chris alikuwa anaoga. Alipomaliza, alijikausha vizuri kisha akajifunga taulo yake kiunoni. Akabeba zile nguo zake na kutoka mle bafuni.

Kwa Laura lilikuwa tukio la ajabu sana. Chris aliingia chumbani na taulo tu. Ajabu kubwa ni Chris kutoka na taulo lakini lingine ni mshangao wa mwili wa Chris.

Kutoka moyoni, Laura alikiri kuvutiwa na mwonekano wa Chris. Taulo lilimfanya mwili wake uonekane kwa ukamilifu wake. Kifua cha mazoezi kilionekana dhahiri, huku tumbo lake likiwa limefunikwa na bustani nzuri ya kupendeza!

Siku zote Laura amekuwa akichanganywa zaidi na miili ya wanaume wa namna hiyo. Shoti ya umeme wa mapenzi ikahamia kwa Laura. Bado alikiri kuwa hajampenda Chris lakini angalau kwa usiku ule angemfaa sana!

“Oooooh! Kumbe yupo hivi? Hebu angalia jamani. Chris ananipa mateso sasa,” akawaza Laura alipomwangalia Chris tumbo lake.

“Samahani kwa mara nyingine, sikujali kutoka na taulo kwa sababu najua hakuna tatizo. Wewe ni rafiki yangu. Au nimekosea?” Chris akasema.

“Uko sawa.”

Chris akafungua begi lake kisha akatoa bukta na tisheti, akarudi tena bafuni. Huko alivaa kisha akarudi tena chumbani. Mawazo yalimjaa Chris. Ni kweli alimtaka sana yule mrembo usiku ule lakini aliogopa angeweza kumkosa kama angemwambia mambo ya mapenzi mapema.

Wazo lake kichwani alijua amepata mke, siyo demu wa kuzugia! Mwisho aliamua kuzishinda hisia zake ili aweze kutengeneza kitu chenye manufaa mengine makubwa zaidi mbele yake.

Angejua!!!

Laura yeye aliumizwa sana na mwili wa Chris. Alitamani sana asikie akimwambia angehitaji kuwa naye usiku ule. Ni kwa usiku ule tu! Laura hakuwa na chembe ya mapenzi ya kudumu na Chris.

Hakuna aliyejua kilichokuwa moyoni mwa mwenzake.

INAENDELEA

No comments

Powered by Blogger.