Simulizi : Singidani Sehemu Ya Tatu (3)

Simulizi ya singidani
ILIKUWA hisia kali za mapenzi lakini kila mmoja alikuwa na hofu ya kumweleza mwenzake kwa hofu ya kuonekana malaya. Chris aliugulia akiwa bado amemkumbatia kwa nguvu akiendelea kuhisi joto zuri la kusisimua la Laura.

Laura aliumia sana, hisia za mapenzi ziliwaka kama moto wa kifuu. Alitaka kusema chochote lakini yeye ni mwanamke; ingewezekanaje? Lilikuwa jambo gumu sana kwake.

Ghafla, kwa msukumo wa hisia ambazo hazikuwa na majibu. Laura alijitoa kifuani mwa Chris. Akasimama hatua mbili kutoka kwa Chris.

“Usiku mwema dada Laura!” Chris akasema kwa sauti ya chini.

“Dada!” neno hilo likajirudia kichwani mwa Laura.

Kuitwa dada pekee kulitosha kabisa kumfanya agundue kuwa, Chris hakuwa akimtaka. Bado moyoni mwake alisimamia jambo moja kubwa; hampendi Chris hata kidogo ila hisia za mapenzi za usiku ule pekee ndizo zilizokuwa zikimpelekesha puta!

Akamwangalia Chris kwa makini, kisha akamwambia: “Hunitoi?”

Lilikuwa swali la mtego sana. Kwa usiku ule, saa tisa kasoro za usiku ilikuwa vigumu kwa mtoto wa kike kutoka mwenyewe katika hoteli ile kubwa. Kutoka kwenye chumba walichokuwepo hadi kufika getini ilikuwa ni mwendo wa dakika tatu, kutokana ukubwa wa hoteli ile.

“Nitakusindikiza usijali. Siyo kukusindikiza tu, nitahakikisha unafika salama.”

“Unamaana unataka kunipeleka?”

“Sina maana hiyo, nitamwita dereva akupeleke.”

Wakatoka nje, Chris akafunga mlango na kuanza kutembea wakiwa wameshikana mikono. Wakiwa katikati ya safari yao kuelekea getini, Chris akatoa simu yake na kumpigia dereva wake aitwaye Maulanga. Akamwambia afike haraka sana Aqua Hotel usiku ule.

Kwa kuwa bado alikuwa Skyway Club, ilikuwa rahisi sana, dakika kumi tu zilitosha kumfikisha Maulanga Aqua Hotel. Chris akamwambia Mulanga ahakikishe anamfikisha Laura anapoishi.

“Mambo ya pesa hayo tufanye kesho lakini hakikisha anafika salama ndugu yangu.”

“Sawa kaka.”

Laura akamsogelea tena Chris ambaye alimvutia kwake. Akamkumbatia na kumbusu. Wakaagana. Akaingia kwenye gari na baada ya muda mfupi sana, Maulanga aliingiza gia namba moja.

Gari likayoyoma!

***

Kwa mbali Chris alijilaumu na kujiona mjinga kwa kumkosa Laura. Taratibu kila kilichotokea chumbani akiwa na mrembo yule, kikaanza kujirudia kichwani mwake.

Kulikuwa na kila dalili za Laura kumwelewa somo lake lakini akajisahau na kuamua kuachana na jambo hilo.

Chris aliumia sana. Hata hivyo alijipa moyo akiamini kwamba, lengo lake hasa halikuwa kumtumia kwa usiku mmoja, bali awe mke wa maisha yake yote.

Jambo hilo ndilo lililompa moyo na kuamini kuwa, bado Laura angekuwa wake! Uchovu wa pombe, mawazo ya mapenzi na baridi kali ya Singida usiku huo, vilimfanya Chris asichukue muda mrefu kupata usingizi!

Akapotelea usingizini.

***

Aliamka akiwa mchovu sana, bado mning’inio wa ulevi uliendelea kumsumbua. Alijimwagia maji kisha akatoka na kwenda mgahawani kupata kifungua kinywa, akarudi tena chumbani kwake.

Kwa kuwa alipanga kusafiri kwenda kijijini Mkalama siku iliyofuata, aliamua kuhama hoteli na kwenda Kibaoni, jirani na Stendi Kuu ya Mabasi ya Mikoani Singida, Misuna.

Maulanga ndiye aliyemsaidia kupata hoteli nzuri iliyokuwa barabara kuu ya Dodoma – Mwanza. Akampigia Laura na kumwelekeza. Akaahidi kufika hapo saa kumi jioni.

***

Laura hakuwa mwongo, alifika pale hotelini kama walivyokubaliana na Chris ingawa alichelewa kwa saa nzima mbele. Alimpigia Chris aliyemwelekeza hadi chumbani kwake.

Akaingia.

Mazungumzo ya hapa na pale yakaendelea, huku jambo kubwa lililotawala likiwa ni kumsaidia Laura ili aweze kuwa msanii mkubwa wa filamu za Kibongo.

Mwisho Chris hakuweza kuvumilia. Mazoea ya muda mrefu yalimfanya amweleze ukweli Laura kuhusu maisha yake yote na lengo la safari yake kuelekea kijijini Mkalama.

“Tafadhali usinifananishe na wahuni, moyo wangu umetuama kwako. Hapa natakiwa kuoa, baba amenipa miezi mitatu tu ya kukamilisha jambo hilo. Najua siwezi kukutana na mwanamke wa hadhi yangu kijijini.

“Nimekupenda wewe na naamini hisia zangu. Ndiyo maana hata jana sikutaka kufanya chochote na wewe kwa sababu najua ninachohitaji kwako ni kikubwa zaidi ya tendo la usiku mmoja tu.

“Tafadhali naomba unisaidie kwa hilo. Nipe nafasi moyoni mwako. Nakupenda sana Laura,” Chris akasema kwa hisia kali sana.

HUMBA kilikuwa kikubwa chenye kila kitu. Giza jepesi la jioni lilianza kuchukua nafasi chumbani mle. Taratibu jua liliendelea kuzama na kufanya ukimya wa jioni uanze kuingia taratibu.

Ndani ya chumba hiki, watu wawili walikuwa wamezama katika mazungumzo muhimu sana. Dk. Chris anajaribu kueleza namna anavyougulia mapenzini kwa msichana mrembo Laura.

Kwa hakika Chris aliamua kujitutumua. Alijihisi mpweke na hakutaka kabisa kumkosa. Tayari alishakatisha safari yake ya kijijini kwao ambako alitakiwa aende kutafuka mke huko.

Laura alimtosha kabisa.

Laura ni kama hakusikia vizuri kauli ya Chris. Kama alisikia basi alikuwa hajaamini maneno ya kijana huyo ambaye anasumbua katika ulimwengu wa filamu za Kibongo.

“Chris una hakika na unachokizungumza?” Laura aliuliza kwa sauti laini, tamu ambayo ilikuwa burudani tosha kwa Chris.

Jibu lilikuwa rahisi sana: “Nina zaidi ya hakika Laura. Nipe nafasi. Nitaumia sana nikikukosa. Moyo wangu umeniambia unakupenda wewe tu. Tafadhali usiniumize wala kuniadhibu.”

“Siamini maneno yako Chris.”

“Kwa nini mama?”

“Sikuamini tu. Nyie wanaume maneno mengi sana, hasa ninyi wasanii. Mh! Hapo utasema maneno yote lakini ukinipata tu, mapenzi yanaishia hapo. Kwa kweli nimeondoa kabisa imani na wanaume.”

“Kuna tofuati kubwa sana kati ya wanaume na Chris. Mimi ni tofauti na wengine wote unaowajua au uliowahi kukutana nao. Mimi ni kweli ni mwanaume, lakini ni Chris. Nipe nafasi tafadhali.”

Kama ni filamu basi Chris alikuwa kwenye kipande cha mapenzi na aliweza kuvaa uhusika wake kisawasawa. Unaweza kudhani hivyo, lakini safari hii Chris hakuwa mbele ya kamera.

Alikuwa akizungumza kutoka ndani na kueleza hisia za kweli za moyoni mwake. Laura alimteka kwa hakika.

“Hata kama nikikubali Chris, kumbuka baba yako ameshasema anataka mke wako atoke kijijini. Angalia... kwanza mimi siishi kijijini, pia siyo Mnyiramba kama baba yako anavyotaka. Mimi ni Msukuma. Itakuwaje?”

“Najua cha kufanya Laura. Ninalo wazo.”

“Wazo gani?” Laura akauliza harakaharaka.

“Lipo lakini nataka kujua kwanza kutoka kwako. Wewe unanipenda?” Chris akamwuliza Laura.

“Ndiyo... kwa nini nimchukie binadamu mwenzangu? Nawapenda watu wote.”

“Tafadhali Laura, usiniumize hisia zangu. Usiutese moyo wangu tafadhali. Nazungumzia mapenzi hapa. Tunajadiliana kuhusu maisha mama. Tafadhali chukulia kwa uzito huohuo Laura.”

“Nakupenda Chris,” Laura akasema mara moja tu, akanyamaza.

“Kweli?”

“Ndiyo... lakini bado kuna mambo nahitaji kuzungumza kidogo na wewe. Kuna vitu nataka kujua zaidi kuhusu wewe. Nadhani tukutane Club jioni, tuzungumze zaidi.”

Chris alisimama alipokuwa amekaa, akapiga hatua fupi nne, akamfikia Laura. Akamnyooshea mikono yake miwili kama ambaye alitaka kupokewa. Laura akaipokea.

Taratibu Chris akamwinua Laura, akasogea mzimamzima. Akamlaza kifuani mwake. Miili yao ikakutana. Wote kwa pamoja wakapata msisimko mkali sana.

“Nakupenda sana Laura,” Chris akatokwa na maneno hayo huku akimwaga machozi.

“Nakupenda pia Chris, sikutegemea kama ningekupenda kwa kiwango hiki. Ngoja niwe mkweli... sikukupenda hata kidogo lakini sasa naona ni kwa namna gani ningepoteza mtu muhimu sana maishani mwangu.

“Nimekupa kila kitu mpenzi wangu. Nakupa moyo wangu. Chukua mwili wangu. Nichukue baba. Nichukue mpenzi. Mimi ni wako kwa kila kitu. Nifanye upendavyo!”

Chris akasisimka!

Sheria yake ilikuwa ileile. Ndani ya nafsi yake, huba zito lilimlemea. Kamwe hakutaka kuonekana mhuni. Pamoja na maneno yale ya Laura kuashiria kwamba alikuwa tayari kwa lolote, moyoni Chris alikataa!

“Ahsante dear. Nami nimekukabidhi kila kitu mpenzi wangu. Nakupenda sana.”

“Nitoe baba niondoke, jioni tukutane Club sawa?”

“Sawa mama.”

Wakatoka nje wakiwa wameshikana mikono. Laura akaingia kwenye taksi na kuondoka zake. Ahadi ilikuwa kukutana Club usiku.

***



ITAENDELEA

No comments

Powered by Blogger.