Simulizi : Singidani Sehemu Ya Saba (7)
“Na hiki kitambulisho cha kura?”
“Angalia nimejiandikishia wapi? Nilishakuambia mimi kwetu siyo Singida, natokea Mwanza. Naona hata kitambulisho changu kimekuthibitishia hilo sasa.”
“Siyo kigezo sana Laura, lakini naomba nikuulize kitu.”
“Uliza tu.”
“Kwanini umekuja Dar?”
“Nimekuja kwa ajili yako Chris. Nakupenda sana, huwezi kuamini jambo hili hasa kutokana na mwanzo wetu ulivyokuwa, lakini nataka uamini kuwa umeingia moyoni mwangu kama cheche za umeme. Unaniumiza baba. Mapenzi yako yananitesa sana ndiyo maana nikaamua kuja hadi huku kwa ajili yako.
“Usinione tapeli au mwenye nia mbaya na wewe, amini moyo wangu baba. Nakupenda sana. Nahitaji kutengeneza familia na wewe. Najua ni kiasi gani una wasiwasi na mimi. Ni haki yako kuwa na mashaka kutokana na mazingira yenyewe na hata mimi niliingiwa na wasiwasi kidogo baada ya kufuatwa na maaskari eti natembea na mume wa mtu.
“Najua ni jambo gumu kidogo kupenya kichwani mwako mpenzi lakini nakuomba sana utambue kuwa moyoni mwangu, mwanaume pekee aliyejaa ni wewe. Niamini na unipe pumziko tafadhali,” Laura alizungumza kwa dakika tatu peke yake bila kupumzika.
Kwa kiasi kikubwa, maneno ya Laura yalimwingia Chris taratibu ubongoni mwake. Alianza kumwamini taratibu kabisa...
“Una uhakika na unayozungumza Laura?”
“Zaidi ya uhakika.”
“Kweli?”
“Niamini.”
Chris alitulia kwa muda tena. Akamwangalia Laura sasa kwa macho ya kawaida yasiyo na hasira. Moyo wake ulilipuka. Laura alikuwa mwanamke mrembo kuliko kawaida. Alihisi mpangilio wa mapigo ya moyo wake ukibadilika kabisa.
Alijilamba midomo yake, akamwangalia kwa makini Laura ambaye sasa macho yake yalishaanza kuchuruzisha machozi mepesi. Chris akasimama na kumshika mikono Laura kisha akamwonyesha ishara asimame. Laura akasimama. Chris kama aliyechanganyikiwa, alimvutia kwake, Laura akaenda mzima-mzima.
Wakakumbatiana!
“Nakupenda sana Laura, nakupenda mama.”
“Nakupenda pia Chris.”
“Tafadhali usiniumize moyo wangu mama, usiniingize kwenye matatizo mama. Isije kuwa unatumiwa na watu ili uniharibie. Tafadhali sana mpenzi wangu, naomba unipende kwa moyo wako.”
“Sijui niseme nini ili uelewe hili ninalosema lakini itoshe tu kukuambia kuwa, linatokea ndani ya moyo wangu!”
Waliangaliana kwa muda mrefu, macho ya wote yakapoteza uwezo wa kutazama vyema, wakakutanisha midomo yao kisha wakaanza kubadilishana mate.
Walidumu katika zoezi hilo kwa dakika mbili nzima, kila mmoja akionyesha hisia kali kwa mwenzake.
“Pwaaaa! Pwaaaa! Pwaaaa! Pwaaaaaaa....” makofi yasikika yakipigwa!
MSHTUKO wa ghafla ukawapata Laura na Chris waliokuwa wamezama kabisa kwenye ulimwengu wa mapenzi. Walikuwa kwenye dunia ya peke yao kabisa, wakiwa hawana habari na watu walikuwa eneo lile.
Makofi yaliyopigwa kama vile watu walikuwa wakishangilia tukio fulani muhimu yaliwachanganya kwa hakika. Haraka wakaachiana. Walishangaa kuona kundi zima la Bongo Film Club likiwa limewazunguka wakiwapigia makofi.
Chris akatabasamu.
“Naomba mnisamehe sana rafiki zangu kwa yote yaliyotokea. Laura, pia naomba unisamehe mama. Ndugu zangu, naomba sasa niwatangazie rasmi kuwa huyu ndiye mama watoto wangu mtarajiwa!” akasema Chris akiachia tabasamu!
Mlipuko wa shangwe ukaendelea.
“Kikao cha kwanza ni wiki ijayo hapa hapa Leaders. Mimi ndiye mwenyekiti na mchango wangu ni milioni tatu,” akasema Jaybee, wenzake wakimshangilia.
“Hayo ndiyo maneno sasa ya kuzungumza... kuhusu usafiri wa maharusi, wazazi na wahudhuriaji wengine kutoka kanisani hadi ukumbini, itakuwa juu yangu,” akasema Chika, wote wakicheka na kuachia shangwe.
Lilikuwa tukio la kufurahisha sana. Jaybee akajitolea ofa ya vinywaji kwa wenzake wote, kisha wakamimina kwenye glasi na kugongesha kwa furaha. Kikao cha kikazi kikabadilika, hawakujadiliana tena kuhusu filamu, walizungumzia ujio wa shemeji yao mpya; Laura.
***
Giza jepesi lilichukua nafasi katika chumba hicho kikubwa chenye hewa safi iliyotoka moja kwa moja kutokea nje kupitia madirisha makubwa mawili kila upande. Pamoja na hewa hiyo nzuri iliyopenya kwenye mapazia mepesi, feni ilisaidia kupooza joto na kuwafanya viumbe hawa kusahau kabisa kama Dar es Salaam ni mji wenye joto kali.
Macho ya Chris yalikuwa yamemwelekea Laura aliyekuwa kitandani na gauni jepesi la kulalia. Chris alikuwa amevaa bukta pekee. Alimwangalia sana kama anayemfananisha na mtu anayemfahamu! Laura alikuwa kimya akijilamba midomo yake.
Hapo sasa, Chris aliamini kweli Laura alikuwa mwanamke mrembo. Macho yake yalizidi kumchanganya Laura na hivyo kushindwa kuvumilia na kumwangushia Chris swali: “Vipi dear, mbona unaniangalia hivyo?”
“Siamini tu kama nipo na wewe.”
“Kwanini mpenzi wangu?”
“Basi tu... sikia darling, kama kuna wanaume wenye bahati duniani, mimi ni mmoja wao. Ni vigumu sana kumpata mwanamke wa ndoto zako katika mazingira kama tuliyokutana mimi na wewe. Kiukweli najisikia faraja sana.”
“Usijali baba, wewe ni wangu, imeshapangwa iwe hivyo.”
“Ahsante mama.”
Chris alivuta shuka, akalitupa juu ya mwili wa Laura, naye akaingia ndani yake. Akamvutia Laura karibu yake, akamkumbatia. Hakuwa na haja ya kuzima, chumba kilikuwa na giza jepesi, mwanga hafifu kutoka taa iliyokuwa nje, ukisaidia kukifanya chumba kiwe katika mwonekano wa kimahaba.
Chris aliuchoropoa ulimi wake kinywani, akausogeza jirani na mdomo wa Laura, kwa fujo akaanza kulambalamba midomo yake. Zoezi hilo halikudumu kwa muda mrefu sana, Chris akaupeleka ulimi wake kinywani mwa Laura, akaupokea!
Hawakuwa na sababu za kuzima taa, mwanga mwepesi kutoka taa iliyokuwa nje ya chumba kile uliwatosha kabisa... wakaamua kuendelea na mambo yao wenyewe!
***
Alihisi mwili wake ukiguswa lakini alifikiri alikuwa ndotoni. Mwili uliendelea kutingishwa kwa kasi, mwisho akaamua kufumbua macho. Alikutanisha macho na uso wa mwanamke mrembo sana; Laura. Kwa mara nyingine aliushangaa uzuri wa Laura.
Laura alikuwa amevaa kanga moja tu kifuani, akionekana alikuwa kwenye pilikapilika za usafi wa asubuhi. Chris alitabasamu, akamwambia: “Vipi dear, umeamkaje?”
“Salama baba, nilikuwa nafanya usafi... nimeshakuandalia kifungua kinywa. Mbona unachelewa sana kuamka? Unatakiwa kwenda kazini.”
“Najua darling, ngoja niingie bafuni nikajimwagie maji kwanza, ahsante sana mpenzi wangu,” akasema Chir.
Haraka akainuka na kwenda bafuni, aliporejea alikwenda moja kwa moja kwenye meza ya chakula.
Wote kwa pamoja wakaanza kupata kifungua kinywa! Uzuri mwingine wa Laura ukaonekana! Alikuwa mtaalamu sana jikoni.
“Mh! Kweli hapa nimepata mke,” akajisemea moyoni mwake Chris.
HISIA za kuwa ndani ya ndoa zilimvamia Chris kwa kasi sana, ni kweli alikuwa anakimbia kuoa muda mrefu kwa sababu hakupata mwanamke ambaye amempenda kwa dhati ya moyo wake, lakini safari hii alikiri kuwa kweli Laura alikidhi vigezo vyote.
“Kama sijawahi kukuambia, naomba nikuambie leo kutoka moyoni mwangu, nakupenda sana Laura,” akasema Chris.
Laura akacheka sana!
“Mbona unacheka?”
“Ni mara ngapi baby umeniambia kuwa unanipenda? Mara nyingi tu... hata jana usiku uliniambia neno hilo.”
“Basi kama ndivyo, naomba nibadilishe maneno, leo utambue kuwa ninasema kwa kumaanisha kuliko siku zote; nakupenda sana Laura, sijajuta kuwa na wewe na kamwe sitajuta mpenzi wangu.”
“Ahsante sana mpenzi wangu kwa maneno yako mazuri.”
Kimya kifupi kilipita, wote wakiendelea kula. Kila mmoja kichwani mwake alikuwa na mawazo yake. Laura alikuwa akiota ndoa na Chris. Kijana mtanashati kama yule, maarufu anayejulikana ndani na nje ya Tanzania kwa kazi yake ya sanaa lakini zaidi ya yote daktari!
Chris yeye alikuwa akifikiria zaidi kuhusu baba yake, ni kweli amempenda sana Laura, lakini maelekezo ya baba yake ilikuwa lazima mkewe atokee kijijini kwao. Tayari alimshamdanganya kuwa mchumba amepatikana kijijini.
“Itakuwaje? Mbona naanza kuona dalili mbaya za kumkosa Laura?” akawaza Chris.
“Lakini nitajua cha kufanya, hawezi kunisumbua. Kichwa changu kinafanya kazi sawasawa,” akajiliwaza kwa maneno hayo.
Ukimya huo wa mawazo ya ndani kwa ndani huku kila mmoja akiwaza lake, ulivunjwa na Laura: “Halafu dear, kuna jambo nataka kukuuliza.”
“Uliza tu mama.”
“Imekuwaje wewe daktari mzima, ukaingia kwenye mambo ya filamu?”
“Kwanza kwa nini umesema daktari mzima? Inamaana hupendi mimi kuwa msanii?”
“Sina maana hiyo mpenzi wangu. Ninavyojua mimi, wengi wanaoingia kwenye sanaa huwa hawana elimu ya kutosha lakini wewe kitaaluma uko vizuri kabisa. Kwa nini sasa ukaingia kwenye filamu?”
“Ni habari ndefu Laura lakini jambo kubwa ambalo nataka kukuambia ujue, napenda sana sanaa na siku zote ndiyo imekuwa chanzo cha ugomvi kati yangu na mzee wangu. Baba alitaka sana niwe daktari, ndiyo maana alinilazimilisha nikazanie masomo ya Sayansi.
“Alijua kunishawishi, kweli nikajikuta taratibu nimeanza kupenda masomo ya Sayansi na nikayamudu vizuri. Baada ya kumaliza kidato cha sita, mzee alinipeleka Uingereza kusomea udaktari. Nimeishi huko kwa miaka saba.
“Pamoja na hayo, bado ndani yangu kulikuwa na chembechembe za sanaa, ndiyo maana nikaamua kurudi nchini kwa lengo hilo, lakini kwa sababu kiu ya mzee ni kutaka kusikia nikiitwa daktari tena nikiwatibu watu, nikaamua kuomba kazi Hospitali ya Kinondoni.
“Mpaka sasa nafanya kazi hapo, lakini nikiendelea na sanaa kama kawaida. Bosi wangu hana tatizo na hilo, maana nilimweleza hali halisi kabla ya kuanza kazi. Naijua vizuri taaluma yangu lakini napenda sana sanaa, vyote vinanipa fedha na ninafanya vyote kwa wakati mmoja,” alisema Chris.
“Hongera yako.”
“Ahsante.”
Walipomaliza kula, wote walitoka kwa pamoja na kuingia kwenye gari la Chris, wakaenda moja kwa moja kazini kwa Chris, akamtambulisha kwa baadhi ya wafanyakazi wenzake kisha akamruhusu aendelee na mizunguko yake mingine.
Laura hakuwa na mambo mengi sana siku hiyo, kikubwa hasa ilikuwa ni kwenda Kariakoo kufanya manunuzi ya mavazi na vitu vingine vya kwenda navyo Singida.
***
Laura alikaa Dar kwa wiki nzima akipoteza vipindi vyote kwa muda huo. Siku ya kurejea Singida ilikuwa ya huzuni sana kwake. Chris alimsindikiza mpaka kituoni, Ubungo ambapo alikuwa ameshamkatia tiketi kwenye basi la ABC.
Laura aliagana na Chris wakiwa wamekumbatiana kwa muda mrefu sana. Ilikuwa ni kama hawakuwa na mpango wa kuachiana. Mwili wa Laura ulisisimka sana, alitamani kuendelea kubaki Dar lakini haikuwezekana, alipaswa awahi masomo Singida.
Muda wa safari ulipowadia, hakuwa na jinsi – aliingia garini na kumwacha Chris akiwa anamtazama kupitia dirishani. Saa 12:00 asubuhi, gari lilianza kuondoka. Laura akampungia Chris mkono huku akitoa machozi, ni kama walikuwa wanarekodi filamu lakini ilikuwa kweli.
Waliendelea kupungiana mikono mpaka gari lilipofika mbali. Chris akaenda kwenye maegesho, akaingia kwenye gari lake, akaondoka. Ilikuwa safari ya kuelekea kazini kwake. Saa 3:00 asubuhi hiyo alikuwa na kazi ngumu sana ya kumfanyia mtu upasuaji mkubwa!
INAENDELEA
No comments