Simulizi : Singidani Sehemu Ya Sita (6)
Ilikuwa Jumamosi, wasanii wengi wa filamu walikuwa wamekaa kwenye viti vya plastiki, pembeni mwa uwanja wa mpira wa pete katika Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni jijini Dar es Salaam. Eneo karibu lote lilikuwa na watu wengi sana.
Mapema sana!
Saa tano asubuhi!
Supu ilinywewa kwa fujo, wengine nyama choma na bia. Kifupi watu walikuwa kwenye mapumziko ya mwisho wa wiki. Wengi wa wasanii wale walikuwa ni wanachama wa klabu yao ya Bongo Film. Wasanii wa klabu hiyo hukutana hapo kila Jumamosi kwa ajili ya kuweka mikakati yao ya kisanii.
Ilibaki nusu saa tu kikao rasmi kianze.
***
Aliteremsha mguu wa kwanza chini kutoka kwenye gari alilokuwa amepanda. Kisha ukafuata mwingine. Baadaye, mwili mzima ulitoka ndani ya gari. Akasimama na kusukuma mlango kwa nguvu wa gari kwa nguvu. Akapunga mkono kumuaga dereva, ambaye aligeuza gari na kuondoka.
Alikuwa msichana mrembo kuliko kawaida. Namna yake ya kutembea ikawa kivutio kingine kwa watu waliokuwa wakimtazama wakati akitembea kwa madaha. Macho yote yalikuwa kwake. Si wanaume wala wanawake.
Wote walishangazwa na uzuri wa msichana yule. Kwa alivyoonekana alijua alichokuwa akikifanya. Alijua alipokuwa anakwenda na alimjua aliyekuwa akimfuata. Alinyoosha moja kwa moja hadi walipokuwa wamekaa wasanii wa filamu.
Wasanii wote wakapagawishwa na uzuri wake. Akasimama katikati yao, akawaangalia kwa zamu, kisha akavua miwani yake myeusi iliyokuwa usoni mwake. Macho yake mazuri yakawa tatizo lingine!
“Samahanini jamani... samahani sana ndugu zangu. Nimekuja hapa kwa sababu ya mtu mmoja tu; Chris!” akasema msichana yule.
Alikuwa ni Laura.
Dk. Chris alishtuka sana alipomuona Laura eneo lile. Akasimama na kumwangalia kwa hasira.
“Kaa mbali kabisa na maisha yangu. Sitaki matatizo. Kama umetumwa, mnajidanganya, mimi ni daktari kitaaluma, tena nimesoma nje ya nchi, mimi siyo bwege!” alisema Dk. Chris kwa hasira.
CHRIS alikuwa anatetemeka kwa hasira. Kichwani mwake aliamini kwamba, Laura alikuwa akimchezea mchezo. Aliamini alikuwa kwenye mtego ili atapeliwe. Hakuwa tayari kwa jambo hilo hata kidogo. Chris alikuwa amefura kwa hasira.
Kitu ambacho hakukijua ni namna msichana yule alivyokuwa akimpenda. Alikuwa akimpenda kwa moyo wake wote, ndiyo maana alifunga safari kutokea Singida kumfuata yeye. Kilichompeleka Dar kilikuwa ni mapenzi tu!
Dk. Chris!
Hilo tu!
Hakutaka kulipa nafasi jambo hilo kichwani mwake. Alidhamiria kukaa naye mbali kabisa. Hisia za mapenzi zilishahama. Hakutaka kumuendekeza. Ramsey rafiki yake kipenzi, akamwangalia yule msichana kwa makini.
Alishawishika sana na urembo wake. Kwa stori za Chris kuhusu mwanamke aliyetaka kumwingiza kwenye matatizo mjini Singida, alianza kuamini kuwa ndiye aliyekuwa mbele yao. Alichokifanya ilikuwa ni kumtuliza rafiki yake kwanza...
“Kaka tulia tafadhali... lakini ni nani huyu msichana?” Ramsey akauliza kwa sauti ndogo.
“Ni yule mwanamke wa Singida niliyekuambia. Anataka kuniharibia maisha yangu huyu. Sikia wewe... umekosea njia, ondoka kwenye maisha yangu,” akasema Dk. Chris kwa hasira na sauti ya juu.
Laura alikuwa analia machozi. Hakuwa anaigiza, alikuwa analia machozi ya kweli kabisa...
Kama angekuwa mbele ya kamera akirekodi filamu, angekuwa amefanikiwa kuvaa uhusika katika kiwango cha mwisho kabisa. Laura aliweza kuonesha kilichotakiwa kufanyika. Lakini haikuwa hivyo... ilikuwa halisi.
Laura alikuwa analilia mapenzi!
“Chris nina kosa gani mimi? Wewe ndiye umekuja kwenye maisha yangu, ukasema unanipenda, nakiri kweli mwanzoni sikuwa na hisia hizo, lakini sasa nimegundua upendo wangu kwako, ndiyo maana nimetoroka chuoni na kuja huku kwa ajili yako.
“Nakupenda Chris. Nakupenda sana baba. Usinifikirie vibaya baba. Ni mapenzi tu. Nakupenda mpenzi wangu. Naomba unipe nafasi, nipe pumziko la moyo ndani yako...” maneno haya yalisikika huku machozi yakiendelea kutiririka machoni mwake.
“Acha uongo wewe... unajifanya mwanafunzi, wewe ni mwanafunzi au mke wa mtu? Nimesema sitaki mawasiliano yoyote na wewe.”
Laura akazidi kulia.
Chika, Katibu Mkuu wa Bongo Film Club, aliingilia kati. Alimshika mkono Laura, akamsihi anyamaze, akatulia kidogo. Chika akaanza kuzungumza: “Maneno ya huyu binti si ya kupuuzwa, anahitaji kusikilizwa. Tafadhali Chris, Ramsey na Jaybee naomba tuzungumze pembeni. Naamini tutapata ufumbuzi.”
“Sitaki!” Dk. Chris akajibu kwa hasira.
“Utataka!” Jaybee, mwenyekiti wa nidhamu wa klabu hiyo alisema.
Dk. Chris akanywea!
Isingekuwa rahisi hata kidogo kumpinga Jaybee, msanii mwenye jina kubwa na sauti Bongo Film Club. Heshima yake ndiyo hasa iliyosababisha akabidhiwe kofia ya kusimamia nidhamu klabuni hapo. Ramsey alijua alichotakiwa kufanya.
Alitoka na kusogea pembeni, Chika akafuta, Jaybee ndiye aliyekuwa wa kwanza akitangulizana na Laura. Dk. Chris akawa wa mwisho. Walitembea mpaka pembeni kidogo na kaunta iliyokuwa ndani. Wakaketi jirani na runinga.
“Wakati mwingine huwa inanilazimu kutumia ukali kidogo ili mambo yaende sawa. Sikuwa na lengo la kukudhalilisha ila nilipenda haya mambo yajadiliwe kwa staha na siri. Chris lazima tuzungumzie huku pembeni,” alisema Jaybee, safari hii kwa sauti tulivu.
“Nimekuelewa...” akasema Chris.
“Huyu msichana unamfahamu?”
“Ndiyo... lakini hafai huyu. Unajua...” akaanza kuzungumza kwa hasira lakini Jaybee akamkatiza.
“Tulia, swali nililokuuliza ni moja tu; unamfahamu?”
“Ndiyo.”
“Utapenda haya mambo tuzungumze pamoja au mtayajadili wenyewe?” akauliza tena Jaybee.
Dk. Chris alitulia kwa muda, alionekana akitafakari jambo kwa kina kidogo. Kichwa chake kilifanya kazi kama umeme. Pamoja na yote hayo, bado hakutaka mazungumzo yale yasikike na kila mtu. Haraka akajibu:
“Nataka tuzungumze mimi na yeye tu!”
“Si unaona mambo hayo?” Chika akasema na wote kwa pamoja wakasimama na kuwaacha Dk. Chris na Laura peke yao.
***
“Nataka uniambie ukweli, umeolewa au hujaolewa?”
Chris akamwuliza Laura.
“Mbona maajabu tena mpenzi wangu? Niolewe na nani sasa?”
“Jibu swali, wewe ni mke wa mtu au sivyo?”
“Sivyo. Sijaolewa mimi.”
“Ndiyo maana nakuambia unataka kunichezea mchezo... mbona mimi nilikuja kutafutwa na maaskari wakisema nimetembea na mke wa mtu... tena mke wa mkuu wa kituo?”
LAURA alihisi kizunguzungu kikali. Yeye awe mke wa mtu? Tangu lini ameolewa? Alihisi kichwa chake kikigonga kwa kasi sana. Ukweli alioujua yeye ni kwamba hakuwahi kuolewa achilia mbali mchumba wa uhakika.
Hakuposwa!
Hakuwa na pete ya uchumba. Hata mwanaume wa uhakika pia hakuwa naye. Ni kweli hakuwa ameolewa. Ilikuwa ni yeye na masomo na starehe tu. Mara chache kuna wakati alikuwa akitoka na wanaume tofauti kwa ajili ya liwazo la moyo wake. Hivyo tu!
Laura alishtuka si mchezo!!!
“Aaaaah! Sasa naanza kupata picha. Hata mimi pia nilifuatwa nikaambiwa kwamba, wewe ni mume wa mtu na mkeo yupo palepale Singida. Nilikwenda hadi kituoni kutafuta ukweli, lakini cha kushangaza, wakasema hakuna kitu kama hicho na wala hakuna maaskari waliotumwa kunitafuta mimi kwa madai ya kutembea na mume wa mtu!” akasema Laura kwa sauti tulivu akionekana dhahiri kuwa na uhakika na alichokuwa akikizungumza...
Chris alibaki mdomo wazi. Hata hivyo, bado hakumwamini Laura hata kidogo.
“Nitaaminije?” akauliza Chris akimkazia macho Laura.
“Subiri,” Laura akasema kwa sauti ya chini.
Alichokifanya ilikuwa ni kufungua pochi yake, kisha akatoa kitambulisho chake cha chuo na kumkabidhi. Baada ya hapo alitoa kitambulisho cha kupigia kura nacho akamkabidhi. Chris akaonekana akivitazama vile vitambulisho kwa makini sana.
“Kwahiyo sasa hii inathibitisha nini?”
“Kwamba mimi ni mwanafunzi wa chuo.”
“Kwani mwanachuo hawezi kuolewa?”
“Anaweza, lakini uliambiwa mimi siyo mwanachuo ni mke wa mtu tu.”
Chris akatulia kwa muda.
ITAENDELEA
No comments