Chombezo : Kivuruge Wa Tandale Sehemu Ya Saba (7)


hadithi nzuri ya kivuruge wa tandale
“Sijambo, shikamoo!” nilimsalimu salamu ambayo haikuwa ikifanana naye huku nikijaribu kuvaa tabasamu la uongo lililochanganyikana na aibu, nikawa nasubiri nione kama ataitikia kwa sababu japokuwa ni kweli alikuwa na pete kidoleni, hakuwa mkubwa sana kwangu kustahili shikamoo.

Badala ya kujibu salamu yangu, aliachia tabasamu lililoshiba kisha akaweka vizuri ‘headphone’ kwenye masikio yake, akageukia dirishani, akawa anatazama nje, nikabaki na maswali mengi sana.

“Kwa nini anacheka?” nilijiuliza moyoni, nikaamua kuachana naye, nikaigeukia simu yangu na kuendelea kufanya kile nilichokuwa nakifanya. Niliendelea kuangalia meseji nilizotumiwa, nikakutana na ya Nancy na ilionesha ilitumwa kama saa nane hivi za usiku.

“Nimefika salama lakini baba kanigombeza sana, kasema kukikucha ana mazungumzo na mimi,” ilisomeka meseji ya Nancy, nikashusha pumzi ndefu na kuendelea kuangalia meseji nyingine.

Kumbe hiyo alinitumia alipofika tu, nikakutana na nyingine ambazo alikuwa akinisifia sana na kunishukuru kwa nilichomfanyia kwa muda mfupi niliokaa naye, akaniambia japokuwa nimemsababishia ‘msala’ kwa wazazi wake, ataumaliza mwenyewe hilo suala, akaniambia tangu awe na akili zake, hajawahi kukutana na mtu aliyemfanya ajisikie kama alivyojisikia muda aliokuwa na mimi.

Nilijikuta nikitabasamu mwenyewe, sijui nini kilinituma nitazame dirishani, macho yangu yakamfuma yule abiria mwenzangu akiwa ‘bize’ kusoma meseji zangu. Alipoona nimemshtukia, alitabasamu tena na kunitazama usoni. Sasa niligundua ni nini kilichomfanya ashindwe kuitikia salamu yangu na badala yake aishie kutabasamu! Kumbe alikuwa akisoma meseji zangu.

Badala ya kukasirika, nilijikuta nikizidi kujisikia aibu, maana kama alikuwa akinifuatilia kuanzia mwanzo, maana yake ameona yote yaliyoandikwa na Madam Bella, Nancy na Salma, tena yote yakihusu kitu kimoja.

Aliendelea kunitazama usoni huku akiwa ametabasamu, na mimi nikawa nimemkazia macho huku nikijaribu kuzificha hisia za aibu zilizokuwa zimenijaa.

“Unaitwa nani?”

“Mimi?”

“Ndiyo, kwani hapa nazungumza na nani?” aliniuliza huku akizidi kunitazama machoni.”

“Ashrafu!” nilimjibu huku na mimi nikizidi kumtazama usoni.

Tukiwa tunaendelea kutazamana, mara redio iliyokuwa ndani ya gari ilianza kupiga wimbo wa Kivuruge wa Nandy. Kiukweli huu wimbo mimi huwa siupendi, si kwa sababu ni mbaya hapana bali ni kwa sababu mara nyingi wadada walikuwa wakitumia maneno yake kunisimanga.

Nakumbuka wakati naachana na Asnath wa Tabata Segerea baada ya kunifuma nikiwa na shoga yake waliyesoma pamoja, Kuruthum, alinitumia meseji kali sana na mwisho eti akaniandikia ‘dedication’ ya wimbo huo wa Kivuruge (nitaeleza baadaye kwa kina kuhusu mimi na Asnath, jinsi tulivyopendana kabla ya baadaye kuja kuishia kuwa maadui wakubwa).

“Umekuwa kivuruge unavuruga sanaaa...” yule dada aliacha kuzungumza na mimi, eti akawa anaimba kwa mapozi kufuatisha muziki huo kwenye redio, huku akinitazama, tabasamu pana likiwa limechanua kwenye uso wake.

Akiwa anaimba, niligundua kitu kuhusu huyu dada! Kwanza alikuwa na meno meupe sana, yaliyopangika vizuri nakumfanya awe na mvuto wa kipekee. ‘Lipstic’ aliyokuwa amepaka ilizidi kumfanya awe na mvuto sana, nikawa namtazama macho yake, nikagundua kwamba pia yalikuwa mazuri!

Sijui ni pepo au ni kitu gani, nilijikuta nikivutiwa naye sana, hata sauti yake ilikuwa ni ile kavu flani hivi, ambayo huwa napenda sana kuisikia masikioni mwangu, basi nikawa namtazama tu anavyoendelea kuimba huku nikijua kabisa alifanya vile kwa makusudi kama anayenipiga kijembe baada ya kusoma meseji zangu.

“Kumbe unajua kuimba vizuri hivyo, itabidi nikupeleke studio,” nilimchombeza, akacheka sana, tayari tulishafika maana konda alipaza sauti akisema hapo ndiyo mwisho wa gari, abiria wengine wakawa wanateremka lakini mimi nikajikuta nikipata uzito na kubaki nimekaa, naye hakuonesha kuwa na haraka sana, akawa amekaa akiwa ni kama anayenisubiri niinuke ili na yeye ainuke.

Ndani ya muda mfupi tu tayari tulishakuwa tumezoeana f’lani hivi, akili fulani ndani ya kichwa changu ikawa inaniambia ‘jaribu kutupia mistari’.


“Twende basi tushuke jamani,” alisema huku akinigusa begani, nikamgeukia nakumtazama, safari hii tukiwa tumesogeleana sana maana alishaanza kuinuka.

“Mbona unaniangalia hivyo mpaka mwenzako najisikia aibu,” alisema huku akijichekesha, nikaona huo ndiyo muda mzuri wa kutekeleza kile ambacho akili yangu ilikuwa ikinituma sana.

“Wewe ni mzuri sana, hivi mumeo huwa anakusifia kila siku kabla hujatoka nyumbani?” nilimwambia, akacheka kwa nguvu na kwa kuwa abiria wote walikuwa bize kuteremka kwenye gari, hakuna aliyemjali sana, nikasimama, na yeye akasimama kwani tayari abiria walikuwa wamepungua sana ndani ya gari.

“Umejuaje kama nina mume?” aliniambia huku akinitazama kwa macho ya bashasha.

“Mwanamke mrembo kama wewe utakosaje mume?” nilizidi kumchombeza, akazidi kufurahi. Miongoni mwa udhaifu mkubwa wa wanawake, huwa wanapenda sana kusifiwa na wajanja kama sisi tunaojua namna ya kuzifikisha hizo sifa zenyewe kwa staili ya kuchombeza, huwa inakuwa rahisi sana kuwanasa.



Hata mwanamke aweje, ukishaanza kumsifia tu, lazima atafurahi, hicho ndicho kilichotokea kwa mwanamke huyu ambaye kama nilivyoeleza, sikuwahi kumuona sehemu yoyote na asubuhi hiyo ndiyo kwanza tulikuwa tumekutana.

Niliposimama, nilitumia ujanja wa kiume wa kumpisha yeye ndiyo atangulie mbele, lengo langu lilikuwa ni kutaka kumtazama vizuri, hasa kwenye ‘plate numbe’ ambao kiukweli umekuwa ugonjwa sugu unaonisumbua.

Nilijikuta nikijishika mdomo kwa mshangao, kwa kuwa muda wote alikuwa amekaa wala sikuweza kumuona yupoje akisimama lakini kumbe alikuwa na umbo ambalo hakuna mwanaume yeyote aliyekamilika anayeweza kupishana naye halafu asigeuke!

Alikuwa amejaaliwa haswaa, nikazidi kuchanganyikiwa na ile nadhiri niliyokuwa nimejiwekea, ya kukaa mbali na mali za watu ikayeyuka kama bonge la mafuta kwenye kikaango.

“Dah! Shemeji atakuwa anafaidi kinoma, kumbe ndiyo umeumbika kiasi hicho,” nilimchombeza wakati akimalizia kushuka ngazi ya mwisho ya gari, alipokanyaga chini, ule mtikisiko ukasababisha ‘msambwanda’ nao utingishike kwa namna iliyoyapa raha ya kipekee macho yangu.

Alicheka na kunigeukia, akanipiga kakibao kepesi begani, tukawa tunatazama huku aibu za kikekike zikiwa zimemjaa usoni.

“Wewe umeniuliza mimi jina, mbona wewe hujaniambia unaitwa nani?”

“Hujaniuliza! Kwani unataka kunijua?” aliniuliza huku tabasamu pana likiwa limechanua kwenye uso wake. Nilichokigundua ni kwamba alikuwa anapenda sana kucheka na kufurahi na katika kipengele hicho, Mungu alikuwa amenipa kipaji cha aina yake maana usingeweza kukaa na mimi halafu usitabasamu au kucheka.

Basi aliniambia kwamba anaitwa Ruqaiya au mama Abdul, akaniambia kwamba anasimamia maduka mawili ya simu ya mumewe yaliyopo mtaa wa Aggrey Kariakoo na kwamba muda huo ndiyo alikuwa akienda kazini.

Sikupoteza muda, nilimwambia mimi ni mtaalamu wa masuala ya kompyuta lakini pia nilikuwa na ujuzi wa ‘kuzi-program’ simu, hasa hizi za kisasa zinapotoka kiwandani, akafurahi sana na kuniambia kwamba eti kukutana kwetu ulikuwa ni mpango wa Mungu.

“Naomba namba yako basi bosi!” nilimwambia, akawa mjanja katika hilo, akaniambia kwamba mimi nimtajie ya kwangu halafu yeye atanipigia.

Mbinu hii huwa inatumiwa sana na wanawake wajanja ambapo badala ya kukukatalia kukupa namba, anakwambia wewe ndiyo umpe halafu anazuga kama anaiandika kwenye simu, ukimpa mgongo tu anaifuta na huwezi kumpata tena, hasa katika mazingira kama yale niliyokutana nayo.

Nilimtajia namba yangu, akaiandika kwenye simu yake kisha akaniaga juu kwa juu huku akionesha kuwa na furaha sana, nilishindwa nifanye nini, nikawa namsindikiza kwa macho akitembea kwa maringo.

Alipopotea kabisa kwenye upeo wa macho yangu, harakaharaka na mimi niliendelea na hamsini zangu, nikakata mitaa na muda mfupi baadaye, tayari nilikuwa nimewasili kazini, nikapanda ngazi mpaka juu, wa kwanza kukutana naye alikuwa ni Salma.

INAENDELEA

No comments

Powered by Blogger.