Chombezo : Kivuruge Wa Tandale Sehemu Ya Kumi na Mbili (12)

hadithi nzuri ya kivuruge wa tandale
Katika suala zima la maneno matamu nilikuwa najijua mwenyewe, kweli nilifanikiwa kumfanya Madam Bella aniamini mno, zile hasira zake zikaisha na sasa tukawa tunapiga stori za hapa na pale, tukifurahi na kucheka lakini yeye akionesha bado kuwa na uchovu wa hali ya juu.

Bado akilini mwangu nilikuwa nawaza nitamtoaje? Bado sikuwa na majibu, nilimpigia simu muuza chipsi ambaye nilikuwa nimezoeana naye, ambaye nikiwa nahitaji chakula huwa nampigia tu halafu ananiletea. Nilimuagiza chipsi kuku mbili na soda kisha nikakata simu, tukawa tunasubiri chakula kije.

“Hivi leo siku gani?”

“Kwa nini unauliza kwa mshtuko namna hiyo?”

“Mungu wangu, nilikuwa nimesahau kwamba leo mjomba ndiyo anakuja kutoka mkoani.”

“Mjomba?”

“Ndiyo, kaka yake mama anakuja kutoka mkoani kwa hiyo inatakiwa nikampokee Ubungo.”

“Sasa ulisahau vipi? Jiandae basi nitakupeleka na gari,” alisema Madam Bella, akawa amenizidi ujanja, niliona mbinu hiyo haiwezekani tena. Hata hivyo, sikutaka kuonekana kama nina njama zangu nyuma ya pazia, nilienda kuoga na muda mfupi baadaye, naye alienda kuoga.

Harakaharaka huku nyuma nilipata wazo, nilichukua simu yangu na kumpigia Nancy. Nilijisikia vibaya sana kumkosea msichana huyu mrembo kwa hiyo nikawa naangalia namna ya kurekebisha makosa.

“Uko wapi?”

“Niko hapa dukani nakusubiri.”

“Sasa sikia, mama mdogo kapata dharura anasafiri, jiandae nitakuelekeza mahali tunapoweka funguo ukapike nyumbani, sawa?”

“Sawa baby!” aliitikia huku akionesha kufurahishwa sana na nilichokisema.


Muda mfupi baadaye, tayari tulikuwa tumeshamaliza kujiandaa, tukatoka na mimi nikafunga mlango, Madam Bella akawa anajinyoosha na kupiga miayo akionesha kuchoka sana.

Baada ya kufunga mlango, funguo niliiweka chini ya ndoo iliyokuwa na mti wa antenna, Madam Bella akanitazama kwa mshangao.

“Mbona unaweka funguo hapo? Ukiibiwa je?”

“Naogopa kutembea nazo maana naweza kuzipoteza ikawa balaa, kuna siku nimewahi kuzipoteza bado kidogo nilale nje, si unaona mlango wenyewe wa chuma huo,” nilimzuga Madam Bella. Kumbe wakati yote hayo yakiendelea, mama mwenye nyumba alikuwa amesimama dirishani kwake akituchungulia.

Sijui nini kilinituma nigeukie kule kwenye dirisha lake, macho yangu na yake yakagongana na katika hali ambayo sikuitegemea, nilishtukia akinikonyeza na kunipiga busu la mbali, harakaharaka nilikwepesha macho yangu maana Madam Bella angeweza kunishtukia.

Tulitoka na kuelekea mpaka pale alipokuwa amepaki gari lake, tukiruka mitaro na madimbwi ya maji machafu, si unajua tena mitaa ya kwetu tandale, wenyeji watakuwa wananielewa ninachokisema.

Njia nzima nilikuwa natafuta njia ya kumkwepa madam Bella kwa sababu licha ya kumseti kwamba nakwenda Ubungo kumpokea mgeni, ukweli ni kwamba hakukuwa na mgeni yoyote isipokuwa nilikuwa nataka kumtoa kijanja ili Nancy aingie.

Unajua kuna kipindi katika maisha, hasa ukiwa kwenye hatua ya ujana, unafanya mambo ambayo baadaye ukikaa mwenyewe na kuyatafakari kwa kina, unashindwa hata kuamini kama ni wewe.

Yaani ndani ya siku moja, tena bado asubuhi kabisa tayari nilikuwa nimewavuruga Madam Bella na mama mwenye nyumba, tena kisawasawa na sasa nilikuwa natengeneza mazingira ya kuwa na Nancy, ungeweza kudhani kwamba ninaongozwa na jini mahaba!

“Umejua kunimaliza! Wewe kivuruge wewe,” alisema Madam Bella huku akinipiga begani, tabasamu pana likiwa limechanua kwenye uso wake, akanibusu kimahaba na kuwasha gari, nikawa nachekacheka mwenyewe, akili yangu ikiwaza mambo mengine kabisa.

“Kuna kitu naomba nikwambie lakini tafadhali usikasirike,” alisema Madam Bella, nikamgeukia na kumtazama usoni wakati akihangaika kulitoa gari pale tulipokuwa tumelipaki.

“Kiukweli mimi nimechoka sana, sidhani kama nitaweza kuendesha gari mpaka Ubungo, isitoshe Barabara ya Morogoro inakuwa bize sana, tusije kuingia kwenye uvungu wa lori bure, naomba kama hutajali nipeleke mpaka kwangu halafu nitakuachia gari ukawapokee wageni,” alisema Madam Bella kwa msisitizo.

Moyoni nilijisikia furaha sana, bado kidogo nishangilie kwa sababu alikuwa amenirahisishia kazi lakini sikutaka kumuonesha, nikavaa uso wa ‘usiriasi’ na kujifanya nampa pole kwa uchovu, akacheka na kurudia kuniambia kwamba eti nimemuweza, tangu apate akili zake hajawahi kusulubiwa kama ilivyotokea siku hiyo.

“Yaani kama isingekuwa hao wageni wako, leo nilitaka tushinde kutwa nzima ndani tu, na hata usiku nisingeondoka, tungelala wote mpaka asubuhi,” alisema huku tabasamu pana likiwa limechanua kwenye uso wake.

Nilishindwa hata nimjibu nini kwa sababu nilijisikia furaha kwa mambo mengi, kwanza kwa mwanamke kama yeye, mzuri, mrembo, mwenye ‘mihela’ yake, kunisifia kwa kiasi kile halikuwa jambo la kawaida. Narudia kusisitiza kwamba licha ya umri wake kusogea, Madam Bella alikuwa mwanamke wa haja haswaa! Aliyeumbwa akaumbika.

Lakini pia nilijisikia vizuri kwa sababu malengo yangu ya kwenda kurekebisha makosa yangu kwa Nancy yalikuwa yakienda kutimia, najua alikuwa amekasirika sana lakini endapo ningepata muda wa kukaa naye, bila shaka angefurahi na kusahau maudhi yote.

Basi nilimwambia asijali sana, yeye akaniache barabarani ninapoweza kupata magari ya Ubungo halafu akapumzike kwa sababu hata kama angesema aniachie gari, ukweli ni kwamba sikuwa najua kuendesha.

Basi alikubaliana na mimi huku akinisisitiza kwamba eti nisikasirike, nikawa nampoza kwa kumwambia kwamba asijali, kila kitu kitakuwa sawa. Alinipeleka mpaka Sinza Kijiweni, akasimamisha gari na kufungua pochi yake, akatoa noti tano za shilingi elfu kumikumi, akaniambia zitanisaidia nauli na mahitaji ya ugeni na kuniambia kwamba nitakwama kwa chochote nisisite kumwambia.

Nilimshukuru sana, akanipiga busu mujarabu, tukaagana akaondoa gari lake na safari ya kuelekea kwake, Mikocheni ikaanza. Nilibaki nimesimama pale kituoni mpaka gari lake lilipopotea kabisa kwenye upeo wa macho yangu.

Kumbe wakati hayo yanaendelea, abiria wengine waliokuwa wakisubiri usafiri pale kituoni walikuwa wakituchora, nilipogeuka nyuma, wanawake watatu wakawa wananong’onezana na kucheka kimbea.

Sikutaka kupoteza muda kuwajali, niliingia kwenye Bajaj na kumuelekeza dereva sehemu ya kunipeleka. Tuliondoka eneo hilo na harakaharaka nilichukua simu yangu nakumpigia Nancy, iliita kidogo tu akapokea, nadhani na yeye alikuwa anasubiri simu yangu kwa shauku.

Nikamwambia kwamba aende pale kwangu, nikamuelekeza na sehemu ya kuchukua funguo, nikashusha pumzi maana sasa nilikuwa na uhakika wa kurekebisha mambo yote hasa ukizingatia kwamba siku hiyo nilikuwa na ruhusa maalum ya kutorudi tena kazini.

Wakati Bajaj ikiendelea kupasua lami, simu yangu ilianza kuita mfululizo, niliitoa na nilipotazama namba, sikuwa nimeisevu. Huwa nakuwa mgumu sana wa kupokea namba ambazo sijazisevu, nikabonyeza kitufe cha kutoa mlio na kuiweka mfukoni, safari ikaendelea.

Muda mfupi baadaye, simu ilianza tena kuita, kutazama namba ya mpigaji ilikuwa ileile, bado sikujisikia kuipokea, nikabonyeza tena kitufe cha kutoa mlio na kuiweka mfukoni.

Iliendelea kuita lakini sikusumbuka nayo tena, nikafika Tandale ambapo nilimlipa yule dereva wa Bajaj fedha zake kisha harakaharaka nikashuka na kuanza kukatiza vichochoro kuelekea nyumbani kwangu.

Kama kawaida yangu, nilipokaribia nilipitia dukani kwa Mangi na kununua ‘busta’ yangu. Nitakuja kufafanua kwa kina kuhusu hii ‘busta’ na jinsi ilivyokuwa inanifanya niwe na ‘stamina’ kubwa uwanjani kiasi cha kumudu kupiga mechi hata na watu wanne kwa siku bila kutetereka.

Nilipomalizana na Mangi, harakaharaka nilielekea nyumbani, nilipoingia tu, mama mwenye nyumba alinidaka juujuu!

“Kuna mtu ulimwambia aje kukufanyia usafi eti?”

“Ndiyo mama, si unajua tena nakosa muda wa kufanya usafi kwa sababu ya ubize wa kazi.”

“Huyu naye ni mpenzi wako si ndiyo?”

“Ha..ha..pana mama!”

“Sikia Ashrafu, nyumba yangu siyo gesti, haiwezekani wanawake wawe wanapishana, mara anaingia huyu, mara yule, sitaki! Nimesema sitaki unanisikia Ashrafu? Haya mtoe haraka kabla sijaingia mwenyewe kumtoa,” mama mwenye nyumba alibwata huku mishipa ya shingoni ikiwa imemsimama.

Nilipigwa na butwaa, iweje aniingilie kwenye mambo yangu binafsi? Lakini kama hiyo haitoshi, kama ishu ni kuonesha picha mbaya pale nyumbani, kwa nini asingeniita tukayazungumza taratibu? Lengo lake la kuniabisha mbele ya mgeni wangu lilikuwa ni nini?

Nilichokigundua ni kwamba alikuwa akilia wivu, tayari alishaanza kunipenda na hakutaka tena kuona mwanamke mwingine akiingia pale ndani! Haya mapenzi ni kitu cha ajabu sana. Basi kwa kuwa tayari nilishaelewa kilichokuwa kinamsumbua, wakati yeye anabwata nilijikaza kiume na kumkonyeza, nikamuona anaanza kubadilika.

INAENDELEA

No comments

Powered by Blogger.