Chombezo : Kivuruge Wa Tandale Sehemu Ya Kumi Na Tano (15)
Alinisogelea na kunibusu kimahaba, akarudia tena kunishukuru na kuniomba eti nisimfikirie vibaya kutokana na jinsi alivyokuwa na hasira mwanzo. Ili kuzidi kumuaminisha kwamba nampenda sana, nilimpelekea vitu vyote muhimu bafuni, akatoka na kwenda kuoga harakaharaka.
Alipomaliza alijiandaa, nikamtoa mpaka barabarani na katika zile fedha nilizopewa na Madam Bella, nilimchomolea shilingi elfu ishirini na kumpa.
“Hizi za nini?”
“Sitakusaidia nauli.”
“Kwani nimekwambia mimi sina nauli,” alisema Nancy huku akionesha dhahiri kutofurahishwa na kitendo cha mimi kumpa fedha.
Inaonesha kabisa malezi aliyolelewa Nancy yalikuwa tofauti mno, hakuwa mwepesi wa kupokea fedha kutoka kwangu, ikabidi kama nilivyofanya usiku ule nilipokuwa namlipia bodaboda, nimlazimishe, akapokea kwa shingo upande.
Basi tuliagana, harakaharaka nikarudi nyumbani, kucheki saa, tayari ilishagonga saa tisa na nusu alasiri, harakaharaka nikaingia bafuni na kujimwagia maji. Nilikuwa nimechoka sana lakini sikutaka kuipoteza bahati ya kwenda kuonana na Ruqaiya, basi nikajiandaa na muda mfupi baadaye, nikiwa nimependeza kisawasawa, nilitoka hadi barabarani.
Kwa kuhofia kuchelewa, niliamua kuchukua bodaboda mpaka Kariakoo, nikamlipa dereva hela yake na kujichanganya kwenye watu wengi, safari ya kuelekea Mtaa wa Aggrey anakofanyia biashara Ruqaiya ikaanza.
“Ashrafuu! Ashraafu!” sauti ya kike ambayo haikuwa ngeni masikioni mwangu ilisikika kutokea nyuma, kabla hata sijajua ni nani, nilijikuta nikikasirika kwa sababu tayari nilikuwa nimeshatoa simu kwa lengo la kumpigia Ruqaiya, kumweleza kwamba nilishafika.
.
“He! Umefika saa ngapi huku?” alisema Nancy, nikajihisi kuishiwa nguvu, nikawa kama mdogo kama Piriton.
“Naongea na wewe Ashrafu, wewe si umekataa kunisindikiza ukanambia huwezi kutoka, imekuwaje tena?” aliniuliza Nancy akiwa amesimama mbele yangu, ikabidi nivue miwani ya jua niliyokuwa nimevaa, nikamtazama huku nikijifanya sina hofu hata kidogo.
“Mbona umepaniki mama, salamu kwanza jamani, kwani mimi na wewe tuna ugomvi?”
“Hapana, nataka unipe ufafanuzi kwanza, sikuelewi!”
“Nilipigiwa simu na bosi akaniambia kuna mtu natakiwa kuja kuonana naye haraka iwezekanavyo kwa sababu usiku wa leo anasafiri kwenda China na kuna mzigo wa kampuni inatakiwa akatuchukulie,” nilidanganya uongo mtakatifu, nikamuona Nancy akishusha pumzi ndefu na kunitazama usoni.
“Na wewe vipi umefikia wapi ishu yako? Umeshaenda kuchukua dawa?”
“Nimeenda ila kuna baadhi ya dawa nimekosa, nimeelekezwa nikajaribu kuangalia kwenye duka moja huku Kariakoo,” alijibu Nancy, ikabidi tusogee pembeni maana msongamano wa watu ulikuwa mkubwa sana kiasi kwamba hata maelewano yetu yalikuwa hafifu.
“Mbona umepaniki sana kuniona?”
“Aah, mi sikuelewi mambo yako ujue,” alisema Nancy kwa sauti iliyoonesha wazi kwamba wivu ulikuwa ukimtesa ndani ya moyo wake.
“Hapa umenikuta niko peke yangu umepaniki hivyo, ningekuwa na mwanamke si ndiyo ungenitafuna nyama kabisa,” nilimchombeza, akatabasamu, nikaendelea kumseti na baada ya dakika chache, tulikuwa tukipiga stori nyingine, akionesha kurudi kwenye hali yake ya kawaida.
“Sasa... naomba basi nikaonane na huyo mtu nisije nikachelewa bure halafu ukawa msala, maana kama bosi ameweza kuninyanyua wakati nilimwambia naumwa, ujue suala lenyewe ni la muhimu sana.”
“Twende wote!” alisema Nancy, akanichanganya kichwa kabisa, ilibidi nibadilike kidogo ili anielewe.
“Nakuomba mama nikaonane naye kwanza, wewe kama unaweza kanunue kwanza dawa halafu nikimaliza nitakupigia simu tuondoke pamoja.”
“Kweli? Isije kuwa unatafuta njia ya kuniacha kwenye mataa,” alisema akionesha kushtukia mchezo kwamba nilikuwa namdanganya, mara simu yangu ikaanza kuita. Kutazama namba ya mpigaji, alikuwa ni Ruqaiya.
“Tena huyo anapiga, please baadaye kidogo mpenzi wangu,” nilimsogelea na kumbusu kwenye paji la uso kisha nikageuka na kuondoka, nikamuacha amesimama palepale huku akionesha kutofurahishwa kabisa na kitendo cha mimi kukataa kuongozana naye.
Japokuwa nilikuwa nimefanikiwa ‘kumtoka’, nilibaki na wasiwasi kwamba huenda akaamua kunifuatilia na kuniharibia mipango yangu. Nilipofika mbele niligeuka na kumtazama, nikamuona akigeuka na kuendelea na ratiba zake, nikashusha pumzi ndefu na kubonyeza kitufe cha kupokelea simu ambayo ilikuwa ikiendelea kuita.
Tayari nilikuwa nimechelewa kwani ilishakata, harakaharaka nikapiga namba ya Ruqaiya, muda huohuo akapokea.
“Uko wapi?”
“Nipo Kariakoo naelekea Mtaa wa Aggrey,” nilijibu, akaonesha kushtuka kidogo.
“Mbona una haraka hivyo? Mi nilikupigia simu nikajua bado uko kwenu Tandale kumbe ushafika?” alisema kwa sauti yake ya masihara, akanielekeza kwamba niende mpaka Mobile Plaza atamtuma mtu aje kunipokea.
Nilienda mpaka kwenye jengo hilo lenye sifa ya kipekee ya kuuza simu za kisasa ghorofa zima, sambamba na vifaa vingine vya kielektroniki, nilipofika mlangoni, nikiwa nashangaashangaa, nilimuona kijana mmoja mdogo wa kiume, akiwa amevalia fulana iliyoonesha ni mfanyakazi kwenye moja kati ya maduka ya simu kwenye jengo hilo.
“Wewe ndiyo Anko Ashrafu?”
“Ndiyo mimi, mambo vipi?”
“Fresh, nimetumwa na bosi nije kukupokea, twen’zetu,” alisema kijana huyo mchangamfu, basi tukaongozana mpaka ghorofani, tukaingia kwenye duka kubwa la simu na vifaa vingine vya kielektroniki.
Kwa mbali nilimuona Ruqaiya akiwa bize na wateja, yule kijana akanionesha sehemu ya kukaa, sikutaka kuonesha shobo kwa Ruqaiya kwa sababu niligundua kwamba kumbe hakuwa mwanamke wa kawaida kama ambavyo nilimfikiria mwanzo.
Unajua mwanzo aliponiambia anasimamia duka la simu la mumewe, nilitegemea kwamba ni yale maduka ya kawaida kama yaliyojaa Mtaa wa Aggrey kumbe ilikuwa tofauti kabisa.
Duka lilikuwa kubwa, tena la kisasa likiwa na vifaa vya mamilioni ya fedha, simu kalikali na juu kulikuwa na runinga kubwa kama tatu hivi, zote zikiwa zimeunganishwa na kuonesha kitu kimoja, nikajikuta nikiingiwa na hofu ndani ya moyo wangu.
Nikiwa bado naendelea kushangaashangaa, nilishtukia nikiletewa glasi ya juisi na mfanyakazi mwingine wa kike, akaniambia eti bosi amesema nisiwe na wasiwasi anamalizia kufunga mahesabu, nilimshukuru na kuinua shingo kumtazama Ruqaiya, akatabasamu na kunikonyeza kiaina, mwili mzima ukanisisimka.
Nilichokuwa nakifikiria ndani ya kichwa changu, ni kwamba Ruqaiya atakaponipa nafasi, nitahakikisha natumia uwezo na maarifa yangu yote kumfurahisha kwa sababu hakuwa mtu wa mchezomchezo. Basi nilitulia pale kwenye sofa nilipokaa, nikawa naendelea kunywa juisi taratibu huku uwezo wangu wa kujiamini ukizidi kupotea.
Ruqaiya alikuwa na kila kitu, mzuri, tena mzuri haswaa, halafu mambo safi. Japokuwa siku zote nilikuwa naamini kwamba bosi wangu, Madam Bella yuko vizuri, kwa Ruqaiya alikuwa hafui dafu.
Basi baada ya kama dakika kumi hivi, Ruqaiya alikuja mpaka pale nilipokuwa nimekaa, yule kijana aliyekuja kunipokea akiwa amembebea mkoba wake. Aliponikaribia, nilimuona kabisa kwamba alikuwa amejawa na bashasha lakini hakutaka watu wengine ndani ya duka hilo waelewe chochote kilichokuwa kinaendelea kati yetu, basi na mimi nikaenda naye sawa.
“Shikamoo bosi!” nilimsalimia kwa adabu, akaitikia kwa uchangamfu huku akinipa mkono, akionekana kujikaza kuzuia kicheko.
“Mbona umechelewa mimi nimeshafunga? Itabidi uje kesho mapema,” alisema huku akinikonyeza kijanja, nikaenda naye sawa tena kwa kumuomba radhi kwa kuchelewa, nikamuahidi kwamba kesho nitawahi asubuhi na mapema.
“Huyu ni ‘patner’ wetu kibiashara, siku nyingine hata kama sipo akija ahudumiwe vizuri,” alisema Ruqaiya kwa sauti ya mamlaka, wafanyakazi zaidi ya sita mle dukani wote wakaitikia na kunikaribisha sana.
Basi aliwaaga, tukatoka dukani na kuingia kwenye lifti mpaka chini, akampokea mkoba yule mfanyakazi na kumwambia wakaendelee na kazi, tukatoka nje kabisa ya jengo hilo, karibu wafanyabiashara wote walikuwa wakimchangamkia Ruqaiya, basi tukaenda mpaka kwenye maegesho ya magari, akabonyeza rimoti yake aliyokuwa ameishika mkononi, gari moja likapiga king’ora na kuwasha taa kisha zikazima.
INAENDELEA
No comments